HabariSiasa

Walivyozimwa kwa minofu

September 4th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WALIOKUWA viongozi wakuu wa upinzani kabla ya handisheki wametajwa kama wasaliti wa mwananchi wa kawaida.

Hii ni baada ya viongozi hao wakiongozwa na kinara wa ODM, Raila Odinga kumezwa na serikali ya Jubilee na hivyo sauti zao kuzimwa.

Wanasiasa hao na wakuu wa mashirika ya umma sasa wanakula ronjoronjo huku maisha ya Wanjiku yakiendelea kuwa magumu kutokana gharama ya juu ya bidhaa, ukosefu wa ajira kwa vijana, ushuru wa juu, ufisadi, madeni, maafisa wa serikali kupuuza sheria miongoni mwa matatizo mengine.

Hali ilibadilika tangu handisheki kwa kile Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga walichotaja kuwa muafaka wa kuunganisha Wakenya.

KUKOSA SAUTI

Kulingana na wadadisi wa siasa, waliokuwa viongozi wa upinzani wakiongozwa na Bw Odinga wamekuwa wakitafuna minofu hivyo kukosa sauti ya kutetea Wanjiku.

“Hakuna mtu anayepiga kelele au kuzungumza akitafuna kwa sababu ni tabia mbaya kufanya hivyo,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa Martin Andati.

“Wamenufaika kwa kuacha kukosoa serikali. Kwa mfano, Bw Odinga ana wadhifa katika AU huku aliyekuwa mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka akiwa balozi wa amani Sudan Kusini. Nyadhifa hizi zina marupurupu,” aeleza mdadisi wa masuala ya kisiasa Tom Maosa.

“Kimya chao sio cha kushangaza. Hawakuwa katika upinzani kwa kupenda au kwa sababu ya imani na misimamo yao. Ni nafasi walikuwa wamekosa ya kufaidika kiuchumi,” asema Bw Maosa.

Anatoa mfano wa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee kutoka Pwani, na majuzi ilifichuliwa kuwa anafaidika kibiashara kupitia kampuni zinazohusishwa na familia yake.

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula pia amenyamaza.

Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Musyoka pia ameacha kukosoa serikali na amekuwa akiwahimiza viongozi kumuunga mkono Rais Kenyatta.

Kimya cha upinzani kilipenya hadi bunge ambapo waliokuwa wakipaza sauti kukosoa serikali sasa ndio wapigaji debe wakuu wa Jubilee.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, John Mbadi amekuwa akisikika tu anapoimba wimbo wa kiongozi wa wengi Aden Duale, tofauti na awali ambapo alikuwa akimkosoa vikali.

Hali ni sawa katika Seneti ambapo James Orengo amekuwa mtetezi mkuu wa serikali ya Jubilee.

Bw Orengo alipata kiti cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti baada ya handisheki kufuatia kubanduliwa kwa Bw Wetangula.

Wabunge wengine ambao wamezima sauti ni Millie Odhiambo (Mbita), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini ), Otiende Amollo (Rarienda), Opiyo Wandayi (Ugunja), Gladys Wanga (Mwakilishi wa Wanawake Homa Bay) na T.J. Kajwang (Ruaraka).

Wadadisi wanasema japo wamekuwa wakidai kwamba waliamua kuunga mkono handisheki ili kutuliza joto la kisiasa, ukweli ni kuwa wanafaidika binafsi ndiposa wakanyamaza.

MANUFAA

Anasema walichofanya wanasiasa wa upinzani ni kujiunga na Bw Odinga ili wapate kunufaika hata kama hawakubaliani na maoni yake.

Sauti za viongozi wa mashirika ya kijamii ambao walikuwa wakikosoa serikali pia zilididimia baada ya muafaka.

Bw Andati anasema wanaharakati wengi walivutwa upande wa serikali na wachache waliobaki wakaingizwa baridi.

Kulingana na ripoti ya Uwazi Consortium iliyotolewa Mei mwaka huu, handisheki ndiyo iliyozima mashirika hayo.

Wanaharakati waliokuwa wakilaumu serikali kama vile Gladwel Otieno wa shirika la AfriCog, George Kegoro na Profesa Makau Mutua wa Kenya Human Rights Commission na Maina Kiai wa InformAction wamekuwa kimya.

Dkt Kennedy Orengo wa Uwazi Consortium alisema japo handisheki ilituliza joto la kisiasa, kwa upande mwingine imelemaza kustawi kwa demokrasia kwani ulimaliza upinzani.