Habari Mseto

Wallah Bin Wallah aikejeli KICD kuruhusu mategu vitabuni

October 18th, 2018 2 min read

Na DENNIS LUBANGA

MWANDISHI wa vitabu vya Kiswahili Wallah Bin Wallah amewaondolea lawama waandishi na wachapishaji wa vitabu, kutokana na makosa katika vitabu viwili vinavyotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi, somo la Kiingereza.

Prof Wallah, badala yake, alilaumu Taasisi ya Kitaifa ya Kukuza Mitaala (KICD) kwa kukosa kukagua vitabu hivyo vilivyochapishwa na shirika la Jomo Kenyatta Foundation kabla ya kuviruhusu kutumiwa na wanafunzi, kabla ya vitabu hivyo kuzinduliwa Januari.

“Kwanini vitabu viandikwe, vichapishwe na vifikishwe shuleni vikiwa na makosa mengi, ilhali tunafahamu kuwa baada ya mtaala mpya kuzinduliwa wachapishaji sasa wanatafuta waandishi mahiri kuviandika? Vitabu hivyo vinafaa kupitia katika mikono ya watu waliohitimu ili kuvikagua, wakiwemo KICD,” Prof Wallah akasema wakati wa kutoa mafunzo kwa walimu wa Kiswahili mjini Eldoret Jumanne.

Alilaumu KICD kwa kukosa kufanya kazi yake namna inavyopaswa, akisema vitabu vyenye makosa vinafaa kuondolewa kutoka kwa wanafunzi kabisa.

“Ikiwa vitabu hivi vimeruhusiwa na KICD, kwanini tuwalaumu wachapishaji ama waandishi. Lawama iko kwa wale ambao waliruhusu vitabu hivyo kutumiwa katika mtaala mpya. “Hatufai kutia ujinga ndani ya watoto wetu, ila tunafaa kuwapa busara.”

Lakini aliwalaumu baadhi ya wachapishaji kwa kuchapisha vitabu visivyoafikiana na viwango vinavyohitajika ili kujitafutia pesa na bila kushughulika na mahitaji ya watoto.

“Kuna baadhi ya wachapishaji ambao huchapisha vitabu kwa nia tu ya kutengeneza pesa bila kujali ubora wa vitabu vyenyewe, lakini bado kuna wengine ambao wanafanya kazi nzuri,” akaongeza Prof Wallah.

Lakini wakijitetea, KICD ilikataa kuwa iliruhusu matumizi ya vitabu hivyo vyenye makosa, ikisema vilitolewa Ghana.

“Tumebaini kuwa ukurasa unaosambazwa ulitolewa kutoka kitabu kinachotumika nchi nyingine. Tunawaomba Wakenya kukagua chanzo cha ujumbe wowote kabla ya kuusambaza,” KICD ikasema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Prof Wallah alikuwa akitoa mafunzo hayo katika Mkahawa wa Pearl, kikao cha siku moja na walimu kutoka eneo la North Rift, kabla ya timu hiyo kuelekea kaunti za Kakamega na Mombasa kwenye msururu wa makongamano mengine.

Meneja wa eneo hilo wa Longhorn Joseph Kuria alisema kuwa timu hiyo inanuia kuwafunza zaidi ya walimu 2,000 wa Kiswahili kote nchini kwa nia ya kuboresha ufunzaji wa somo hilo.