Makala

WALLAH: Umoja huwa nguvu imara kuliko nguvu za kutumia kifua

October 15th, 2020 2 min read

NA WALLAH BIN WALLAH

MAHALI palipo na umoja pana amani. Na palipo na amani pana nguvu na maendeleo. Umoja ndio nguvu imara kuliko nguvu za kutumia kifua na silaha.

Wanyamapori wanayamudu maisha yao ya kuishi porini kutokana na umoja wao. Wao hutembea pamoja na kutafuta malisho kwa makundi! Adui anapokuja kuwavamia, wanyama wote hukimbia pamoja kuelekea upande mmoja. Mwenzao anayejitenga kukimbia peke yake kuelekea upande tofauti ndiye huandamwa na adui hatimaye hukamatwa kwa urahisi!

Sisi binadamu na akili zetu alizotujalia Mwenyezi Mungu, tuna umoja kweli? Tunatumia nguvu nyingi za vifua ambazo wakati mwingine hazitusaidii kujilinda adui anapokuja! Kwani hatujui kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu?

Siku moja nilimsikia Mzee Pepeta akisema kwamba, “Kila mtu anajua njia lakini wote hawafuati njia!” Sasa kuna faida gani kujua njia iliyo salama bila ya kuifuata ili uende penye usalama? Kuna mantiki gani wanadamu kujua kwamba umoja ni nguvu kisha waendelee kuishi kwa kutengana kama ardhi na mbingu?

Mzee Pepeta alikuwa na watoto sita. Wasichana watatu na wavulana. Wote walisoma wakahitimu vizuri sana katika masomo yao.

Pamoja na elimu yao nzuri, kila mara Mzee Pepeta aliwakumbusha watoto wake kuishi kwa umoja na amani bila wivu wala chuki. Aliwahimiza washirikiane na kushikamana kama jembe na mpini! Alisema, “Wanangu, palipo na umoja pana amani na upendo! Umoja una nguvu kama ukuta wa zege ambao haubomoki kwa urahisi!” Mzee Pepeta alitoa nasaha!

Hatimaye Mzee Pepeta alipohisi kuwa siku zake za kuishi duniani zakaribia ukingoni, aliwaita wanawe wote sita katika ukumbi wa nyumba yake.

Baada ya salamu za heshima kwa baba yao, watoto waliketi! Mzee Pepeta alifungua shubaka akatoa vijiti sita vyembamba vilivyofungwa pamoja vyenye urefu wa sentimita ishirini hivi! Akawaambia watoto hao, “Kila mmoja ajaribu kuvunja vijiti hivyo vikiwa pamoja!” Kila mtoto alijaribu kwa nguvu zake zote lakini hakuna aliyeweza kuvivunja vijiti sita vilivyofungwa pamoja!

Mzee alivifungua vijiti vile akampa kila mtoto kijiti chake akishike mikononi! Akawaambia, “Sasa kila mmoja akivunje kijiti chake!” Kila mtoto alikivunja kijiti chake kimoja kwa urahisi na wepesi kama mchezo tu! Mzee Pepeta akawaambia wanawe, “Naam, hiyo ndiyo siri ya umoja na udhaifu wa utengano! Nyinyi pia wakati mtakapotengana, walimwengu watawavunja haraka sana kama mabua ya mahindi!” Umoja ndio nguvu za kweli kuliko nguvu za kutumia kifua!” Wazalendo wote tushikane tuwe na umoja katika nchi yetu bila kutengana! Umoja ndio nguvu!!!