Habari MsetoSiasa

Waluhya kuongoza Kenya ni ndoto – Khalwale

May 20th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA seneta wa Kakamega Boni Khalwale, ambaye aligeuka mfuasi sugu wa Naibu Rais William Ruto sasa anasema umoja wa Waluhya ni ndoto, wala hakuna kiongozi kutoka eneo la magharibi mwenye uwezo wa kuongoza Kenya.

Akizungumza eneo la Bumula, siku moja tu baada ya kugura chama cha Ford Kenya na kujiunga na Jubilee, Dkt Khalwale alisema aliamua kujiunga na Jubilee baada ya kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kukosa kusikiza ushauri wake, kuhusu mpango mwafaka wa kushinda.

Dkt Khalwale alisema Bw Wetang’ula pamoja na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi walikataa kumsikiza alipopendekeza wote wavunje vyama vyao na kumuunga Dkt Ruto, akisema tayari alikuwa ameona hawatashinda kitu 2022.

“Ndugu zangu hao wawili walikataa na kushikilia kuwa sharti wawe debeni 2022, lakini baada ya kuwapima nikaona hawawezi kushinda kitu,” akasema mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa mtetezi mkuu wa umoja wa waluya kabla ya kunyakuliwa na Naibu Rais.

Alisema sasa hafai kulaumiwa kwa kuwa ameona mwanga kwa kujiunga na Dkt Ruto ambaye ndiye atashinda Urais 2022.

Kiongozi huyo alisema kuwa jamii ya Waluya imekuwa upinzani miaka kumi na hivyo hangeketi akitazama ikielekezwa upinzani tena kwa muhula mwingine.

“Ruto ndiye mwaniaji aliye katika nafasi bora kushinda uchaguzi 2022, kwa hivyo tusiendelee kudanganywa tukaishia kukaa kwenye baridi miaka yote,” akasema Dkt Khalwale.