Waluke ajisalimisha kwa polisi kupelekwa jela

Waluke ajisalimisha kwa polisi kupelekwa jela

NA RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Sirisia John Waluke leo Ijumaa amejisalimisha kwa polisi katika Mahakama Kuu ya Milimani baada ya kujificha siku moja.

Waluke amepelekwa moja kwa moja hadi gereza la Viwandani kuanza kutumikia kifungo cha miaka 67 baada ya kupatikana na hatia ya kuilaghai serikali zaidi ya Sh297 milioni katika kashfa ya mahindi mwaka 2004.

Waluke alifika katika jengo la Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi mwendo wa saa saba kasoro dakika 20.

Mbunge huyo alifika kortini akiwa ameabiri gari la teksi na kufululiza moja kwa moja hadi seli zilizo katika mahakama ya Milimani.

Akiwa amevalia kofia iliyofunika uso, Waluke alionekana akicheka huku akijisalamisha kwa afisa mkuu wa Polisi Mahakama ya Milimani.

“Waluke amejisalamisha kwa polisi wanaohudumu katika Mahakama Kuu Milimani,” afisa anayesimamia kituo cha polisi idara ya mahakama (JPU) Lazarus Opicho amethibitishia Taifa Leo.

Bw Opicho amesema Waluke alikabidhiwa askari jela waliompeleka kuanza kutumikia kifungo kama ilivyoagizwa na Jaji Esther Maina mnamo Oktoba 6, 2022.

Waluke alitoroka kortini kabla ya polisi kumkamata wakati Jaji Maina alitupilia mbali rufaa aliyokata mwanasiasa huyo.

Jaji huyo alitupilia mbali rufaa walizokata Waluke na mfanyabiashara mwenzake Grace Wakhungu waliohukumiwa na hakimu mkuu Elizabeth Juma kwa kuilaghai serikali Sh297,386,505 katika kashfa ya mahindi.

Wote wawili walikuwa wamefika kortini Alhamisi kujua hatma ya rufaa waliyokuwa wamekata.

Rufaa zao zilitupiliwa mbali kisha Jaji Maina akaamuru wawili hao wapelekwe gerezani.

Jaji Maina alifutilia mbali dhamana zao kisha maafisa wa polisi wakamshika Grace, lakini Waluke akaponyoka hadi leo Ijumaa alipojisalamisha kwa polisi.

Waluke pamoja na mkurugenzi mwenzake katika kampuni ya Erad Supplies & General Contractors Limited, Grace Wakhungu, walianza kutumikia upya vifungo vya miaka 67 na 69, Jaji Maina alipotupilia mbali rufaa zao. Walikuwa nje kwa dhamana.

Punde tu Jaji Maina alipokataa kuharamisha vifungo hivyo, maafisa wa idara ya magereza na polisi walimtia nguvuni Bi Wakhungu, lakini Waluke akatoweka.

Waluke alikuwa amekaa ndani ya gari lake uamuzi ulipokuwa ukisomwa kwa njia ya mtandao (virtual).

“Mtaniangusha mking’ang’ana kunipiga picha,” Bi Wakhungu aliwalalamikia wapiga picha kutoka vyombo mbali mbali vya habari.

Katika uamuzi aliotoa Alhamisi, Jaji Maina alisema adhabu aliyotoa hakimu mkuu Elizabeth Juma ilikuwa inaambatana na sheria na aliwapata na hatia ipasavyo katika kesi ya ufisadi wa kuilaghai NCPB Sh297,386,505.

Jaji Maina alisema wawili hao waliifuja NCPB mamilioni hayo ya pesa wakidai kampuni yao ilikuwa imeingiza nchini tani 40,000 za mahindi 2004.

Kulikuwa na uhaba wa mahindi mwaka huo kutokana na kiangazi kikali kilichokumba nchi.

NCPB ilitoa tenda ya kuingizwa tani 180,000 kutoka ng’ambo.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa na wafungwa hawa hii mahakama imefikia uamuzi kwamba rufaa zao hazina mashiko kisheria na zimetupiliwa mbali. Mashtaka dhidi yao yalithibitishwa kabisa,” alisema Jaji Maina.

Baada ya kufikia uamuzi huo mahakama iliratibisha vifungo hivyo na kuwaamuru wafungwa hao wasitumikie ama walipe faini walizotozwa.

Waluke aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita Agosti 9, 2022 kwa tikiti ya chama cha Jubilee aliagizwa alipe faini ya Sh727,725,562 ama atumikie kifungo cha miaka 67.

Bi Wakhungu aliamriwa alipe Sh707,725,562 ama atumikie kifungo cha miaka 69.

Mahakama ilisema wawili hao walighushi cheti cha kudai malipo kutoka NCPB kuhusu uigizaji na uhifadhi wa mahindi kutoka ng’ambo.

“Waluke alimkabidhi cheti cha kulipwa mwamuzi wa mzozo kuhusu malipo ya mahindi hayo kati ya Erad na NCPB akijua barabara kampuni yao Erad Supplies & General Contractors Limited haikuwa imehusika kamwe kisha akapokea malipo,” alisema Jaji Maina.

Wakurugenzi hao (Waluke na Wakhungu) walipatikana na hatia katika mashtaka matano ya kutegemea cheti ghushi kudai malipo, kujitajirisha kimakosa na pesa za umma na kutoa habari za uwongo mbele ya mwamuzi wa mzozo wa malipo hayo kati ya Erad na NCPB.

Waluke na Wakhungu walifanya uhalifu huo kati ya 2009 na 2013.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Alexander Muteti uliita mashahidi 27 kuthibitisha kesi dhidi ya mwanasiasa huyu na Wakhungu.

You can share this post!

Yaya asukumwa jela miaka 5 kwa kumlisha mtoto kamasi

Mhariri wa KBC apata afueni kesi ya kusukumwa jela

T L