Waluke atorokea bungeni yeye na Wakhungu wakirudishwa jela miaka 67 na 69 mtawalia

Waluke atorokea bungeni yeye na Wakhungu wakirudishwa jela miaka 67 na 69 mtawalia

NA RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Sirisia John Waluke amerudishwa tena gerezani baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali rufaa aliyokata kupinga kifungo cha miaka 67 alichohukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuilaghai Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) Sh297 milioni miaka tisa iliyopita.

Bw Waluke pamoja na mkurugenzi mwenzake katika kampuni ya Erad Supplies & General Contractors Limited Grace Wakhungu walianza kutumikia upya vifungo vya miaka 67 na 69 Jaji Esther Maina alipotupa rufaa walizokata kupinga adhabu hizo.

Punde tu Jaji Maina alipokataa kuharamisha vifungo hivyo maafisa wa idara ya magereza na polisi walimtia nguvuni Bi Wakhungu lakini Bw Waluke alichomoka kutoka egesho la mahakama ya Milimani na kutoweka. Waluke alikuwa amekaa ndani ya gari lake uamuzi ulipokuwa ukisomwa kwa njia ya mtandao (virtual).

“Mtaniangusha mking’ang’ana kunipiga picha,” Bi Wakhungu aliwalalamikia wapiga picha kutoka vyombo mbali mbali vya habari.

Wanahabari walikimbia kupiga picha walipoona maafisa wa polisi na askari jela wakimpeleka Bi Wakhungu seli kabla ya kupelekwa gereza la Lang’ata.

Bw Waluke na Bi Wakhungu walikuwa wamefika mahakama ya Milimani jijini Nairobi wakati wa kusomwa kwa uamuzi wa rufaa ya kupinga adhabu ya vifungo vya miaka 67 na 69 mtawalia na hakimu mkuu Bi Elizabeth Juma mwaka 2021.

Katika uamuzi aliotoa leo Alhamisi, Jaji Maina amesema adhabu aliyotoa hakimu mkuu Elizabeth Juma ilikuwa inaambatana na sheria na aliwapata na hatia ipasavyo katika kesi ya ufisadi wa kuilaghai NCPB Sh297,386,505.

Jaji Maina amesema wawili hao waliifuja NCPB mamilioni hayo ya pesa wakidai kampuni yao ilikuwa imeingiza nchini tani 40,000 za mahindi 2004. Pesa walichukua mwaka 2014.

Kulikuwa na uhaba wa mahindi mwaka huo kutokana na kiangazi kikali kilichokumba nchi.

NCPB ilitoa tenda ya kuingizwa tani 180,000 kutoka ng’ambo.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa na wafungwa hawa hii mahakama imefikia uamuzi rufaa zao hazina mashiko kisheria na zimetupiliwa mbali. Mashtaka dhidi yao yalithibitishwa kabisa,” amesema Jaji Maina.

Baada ya kufikia uamuzi huo mahakama iliratibisha vifungo hivyo na kuwaamuru wafungwa hao wasitumikie ama walipe faini walizotozwa.

Waluke aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita Agosti 9, 2022 kwa tikiti ya chama cha Jubilee aliagizwa alipe faini ya Sh727,725,562 ama atumikie kifungo cha miaka 67.

Bi Wakhungu aliamriwa alipe Sh707,725,562 ama atumikie kifungo cha miaka 69.

Mahakama ilisema wawili hao walighushi cheti za kudai malipo kutoka NCPB kuhusu uigizaji na uhifadhi wa mahindi kutoka ng’ambo.

“Waluke alimkabidhi cheti cha kulipwa mwamuzi wa mzozo kuhusu malipo ya mahindi hayo kati ya Erad na NCPB akijua barabara kampuni yao Erad Supplies & General Contractors Limited haikuwa imehusika kamwe kisha akapokea malipo,” alisema Jaji Maina.

Wakurugenzi hao (Waluke na Wakhungu) walipatikana na hatia katika mashtaka matano ya kutegemea cheti ghushi kudai malipo, kujitajirisha kimakosa na pesa za umma, na kutoa habari za uwongo mbele ya mwamuzi wa mzozo wa malipo hayo kati ya Erad na NCPB.

Mbunge wa Sirisia John Waluke. PICHA | MAKTABA

Waluke na Wakhungu walifanya uhalifu huo kati ya 2009 na 2013.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Alexander Muteti uliita mashahidi 27 kuthibitisha kesi dhidi ya mwanasiasa huyu na Wakhungu.

Kesi hiyo pia ilijadiliwa katika kamati ya bunge kuhusu matumizi ya pesa za umma.

Kamati hiyo ya bunge ilifikia uamuzi pesa za umma zilifujwa.

Mahakama ilisema kesi iliyowakabili wakurugenzi hao wa Erad ni mbaya na walijinufaisha kimakosa kwa pesa za umma.

Mahakama ilisema wakurugenzi hao walitumia makaratasi feki kudai malipo kutoka NCPB.

  • Tags

You can share this post!

Vivian Nasaka Makokha ajiunga na Hakkarigucu Spor kwa...

Sakaja aisihi serikali kukumbuka Nairobi katika ugavi wa...

T L