Makala

Wamagata abaki kushangaa panya na nguruwe si kitu kwa wabunge

September 14th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MWANAHARAKATI John Wamagata ana tangazo ambalo sio la kibiashara bali – kwa maneno yake – ni la kutetea haki za Mkenya ambaye amegeuzwa kuwa ng’ombe wa kuvamiwa na kupe kwa maana ya viongozi walafi.

Ameghasika akisema kwa sasa hakuna lingine ila tu kujitokeza kwa nguvu zake zote mitaani hasa karibu na majengo ya bunge la kitaifa na kuwaaibisha wabunge ambao wamechukua mfano wa jadi kutoka kwa wenzao wa kujipa nyongeza za marupurupu na mishahara katika kila mwanya wa utawala.

“Haiwezekani sasa! Wametuzoea sana na hata wakati nimewavamia nikitumia nguruwe, panya na punda, bado wamenionyesha kuwa hawajali. Ninakusudia kufanya kitu tofauti mara hii,” akasema Wamagata wakati akipinga njama yao ya kujipa marupurupu ya ziada nje ya udhibiti wa tume ya kutathmini mishahara na marupurupu (SRC).

“Tukatae hata hii hazina yao ya ustawishaji maeneobunge (NGCDF) kwa kuwa katika Katiba hakuna mahali wamepewa ruhusa ya kuratibu pesa, tukatae njama za kubadilisha katiba bila kutuhusisha kama wadau wakuu wa kutawaliwa na la muhimu, hawa watu watuheshimu,” akasema.

Katika hali hiyo, anasema kuwa uvamizi wa panya na nguruwe kwa sasa hauna uzito wa kuonyesha vile anachukia tabia ya hawa wabunge.

“Hivi karibuni nitatua katika majengo hayo ya bunge nikiwa na wanaharakati wenzangu na ambapo tutakuwa tumebeba karatasi shashi kupitisha ujumbe kuwa raia sio kifaa cha kutumia kujipangusa uchafu,” akasema.

Anasema kuwa ameunda vuguvugu la Toilet Paper Movement Kenya na ambapo nia kuu ni kujiangazia kama wanaodharauliwa na wabunge kiasi cha kutumiwa tu wakati kuna “haja kubwa ya kuwapa afueni tumboni.”

“Hiyo afueni ya tumboni ni ulafi; washibe na chakula kikishaorodheshwa kwa msingi wa kile cha kufaa mwili na cha kutoka, wakijisaidia haja kubwa ndipo wanatuhitaji tuwabebee hicho kinyesi chao tukakitupe,” aeleza Wamagata.

Huyu Wamagata ashawahi kuwania kiti cha ubunge Kabete katika uchaguzi mdogo wa 2014 na ambapo alishindwa na Ferdinand Waititu ambaye hatimaye mwaka wa 2017 alichaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu.

Aidha, anasema kuwa harakati hizo zitaimarishwa hadi katika serikali za kaunti ambapo wote wa ulafi watapata adhabu sawa.

Hata hivyo, kuna sheria za kudhibiti umwagaji taka nchini, hasa mijini na kunahitajika vibali tele vya kuzingatia usalama wa kiafya kwa umma katika harakati za utupaji taka hiyo.

Hili huenda likamkanganya Wamagata na washirika wake wakijieleza kupitia vuguvugu la Toilet Paper Movement Kenya.

Hata hivyo, pia kuna haki za kujieleza kupitia maandamano na ambapo Wakenya wakiwa ndio wamepewa idhini kuu na Katiba yao ya kujiamlia jinsi ambavyo wanaweza kuendesha masuala yao.

Pengine wakikongamana na waamue mikakati ya Toilet Paper Movement Kenya ndiyo kielelezo tosha cha kutoa hisia zao, huenda; kwa umbali ifahamike, Wamagata akapata mwanya wa kufaulu katika azma yake.

Hii ni dunia iliyojaa viroja!