Makala

WAMALWA: Matokeo ya KCPE yawe msingi wa makuu ya baadaye

November 28th, 2018 2 min read

NA STEPHEN WAMALWA

HONGERA kwa wanafunzi 1,052,364, wavulana 527,294 na wasichana 525,070 waliofanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) mwaka 2018.  Ninyi ni fahari yetu.

Matokeo ya mwaka huu yalimridhisha kila mdau wa elimu hasa baada ya zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi kupata zaidi ya alama 250.

Nilifuatilia hafla ya kutangazwa kwa matokeo haya na kujihisi mwenye furaha kuona utendakazi mzuri wa wadogo wetu.

Nilimtazama waziri wa elimu Amina Mohammed akiyasoma matokeo haya na kugundua kuwa pia alikuwa na furaha. Ilimwia vigumu kwake kuificha tabasamu yake.

Takriban wanafunzi 12,273 walipata zaidi ya alama 400, wanafunzi 228,414 wakapata kati ya alama 300 na 400, wanafunzi 574,927 walipata kati ya alama 200 na 300 na wanafunzi 234,573 wakapata kati ya alama 100 na 200.

Idadi ndogo ya wanafunzi 2,177 ndio iliyopata alama chini ya 100. Ninaamini kuwa chanda cha kila mmoja wenu kitatiwa pete kutokana na juhudi hizi.

Ninafahamu kuwa wanafunzi waliopata alama chini ya 250 huenda wanajihesabu kuwa walioshindwa. Hili si kweli na wala nyota zenu hazijazima ng’o!

Muulize Dkt Purity Ngina kutoka kaunti ya Nyeri. Dkt Ngina alipopata alama 235 baada ya kufanya mtihani wake wa darasa la nane miaka michache iliyopita, yeye hakuwahi kufikiri kuwa angeibuka kuwa msomi mchanga zaidi kuwahi kutuzwa shahada ya uzamifu.

Hakuwahi kujua kuwa ataibuka kuwa msomi maarufu mchanga wa somo la hisabati.

Hata hivyo, alipopata alama hizi, mamake sawa na walivyo baadhi ya wazazi wenu sasa alighadhabika na kumtaka arejee darasa la nane kujaribu tena. Alhamudululahi! Baada ya mwaka mmoja hatimaye alipata alama 368 na kujiunga na shule ya upili ya Tumu Tumu katika kaunti yaNyeri.

Baadaye alipata alama ya B+ na kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton kwa shahada ya kwanza kusomea hesabu. Huku alikaza kamba, alikwangura shahada ya juu kabisa (First Class Honours) iliyomwezesha kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili na hatimaye uzamifu.

Sasa ni daktari baada ya juhudi za kipindi kifupi japo chenye uhitaji wa kujituma.

Ni muhimu kutafakari matokeo yenu kwa kuongozwa na walezi wenu. Yapo matumaini ya kuwa mnachopenda. Ndiyo kwanza chombo kinang’oa nanga bandarini kwa safari ndefu na tamu ya masomo.

Jifungeni kibwebwe mkatimize ndoto za maisha yenu ishallah za kuwa watu wenye faida kwa jamii ya siku zijazo.

 

Mwandishi ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika nchini Uchina.

[email protected]