Wamaragoli wanaoishi Uganda watarajiwa kutambuliwa rasmi

Wamaragoli wanaoishi Uganda watarajiwa kutambuliwa rasmi

Na BAMUTURAKI MUSINGUZI

BAADA ya miongo kadhaa ya kuishi vivulini katika taifa ambalo wamelifahamu kama nyumbani, wanajamii wa Maragoli, ambalo ni kundi la wachache, hivi karibuni watatambuliwa kama miongoni mwa makabila 65 ya Uganda, katika marekebisho yaliyopendekezwa kuhusu Katiba ya Uganda ya 1995.

Idadi halisi ya Wamaragoli nchini Uganda haijatolewa wazi ila imezingatiwa miongoni mwa “wengine” katika shughuli mbili za hivi majuzi za hesabu ya watu, kulingana na Kundi la Kimataifa kuhusu Haki za Wachache (MGR).

Viongozi kutoka Wilaya ya Kiryandongo na jamii katika eneo la Bunyoro, katikati mwa Uganda Magharibi, wanakadiria idadi ya wanajamii wa Maragoli kuwa kati ya 25,000 na 30,000.

Idadi kubwa ya wanajamii hao wanapatikana katika Wilaya ya Kiryandongo ambapo makazi yao yanachukua angalau parokia mbili zinazojumuisha vijiji viwili au vitatu.

Baadhi wametawanyika eneo la Kigumba, mji mkuu wa Wilaya ya Kiryandongo.

Kulingana na MRG, Wamaragoli wameishi Uganda kwa zaidi ya karne moja na hadi hivi majuzi, wamekuwa wakikabiliwa na matatizo machache sugu ama na jamii wanazoishi nazo au serikali.

Ingawa hawakujumuishwa katika ratiba ya Katiba 1995 na ratiba iliyorekebishwa katika marekebisho ya kikatiba 2005, inayoorodhesha makabila ya Uganda, wameendelea kufurahia haki sawa na raia wengine.

Matatizo yanayokumba Wamaragoli kwa sasa yalianza mnamo 2015 wakati serikali nchini humo ilipoanzisha shughuli ya kuwasajili raia wote wa Uganda na kumpa kila mmoja kitambulisho kwenye mfumo mpya uliobuniwa wa Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Vitambulisho na Usajili (NIRA).

Ni wakati huo ambapo jamii hiyo ilijipata kwa mara ya kwanza katika hatari ya kukosa taifa kutokana na vitambulisho vyao kuzuiliwa, kulingana na MRG.

Mnamo 2017, NIRA ilizuilia vitambulisho 15,000 vya wanajamii wa Maragoli kwa misingi kuwa hawatambuliwi kama kabila la Uganda.

Mbunge anayeondoka wa Kibanda Kusini, Wilaya ya Kiryandongo, Jack Odur Lutanywa, mnamo Agosti 2020 aliwasilisha Bungeni mswada wa mwanachama wa siri kuhusu Marekebisho ya Katiba Nambari 20, 2020, akitaka kutambuliwa kwa Wamaragoli kama mojawapo wa makabila ya Uganda.

Lengo la Mswada huo ni kurekebisha Awamu ya Tatu ya katiba ili kuwajumuisha Wamaragoli waliohamia Uganda katika Karne ya 18, kama mojawapo wa jamii za kale Uganda mnamo Februari 1, 1926.

Awamu ya Tatu ya Katiba inatoa orodha ya makabila 65 ya kale yanayostahili uraia kwa misingi ya kuzaliwa kwa sababu jamii hizo zilikuwa zikiishi Uganda kufikia Februari 1, 1926.

Lutanywa alihoji kuwa maadamu Wamaragoli walikuwa nchini humo kabla ya Februari 1926, Uganda ilipobuniwa, wanastahili kutambuliwa kama wenyeji.

Alieleza kwamba wanajamii hao tangu 1990, wamekuwa wakiomba kujumuishwa katika katiba kupitia mawasilisho Bungeni, kwa mawaziri na idara mbalimbali za wizara za Rais Museveni bila mafanikio.

Waelezea changamoto zao

“Changamoto yetu kuu kwa sasa imekuwa kukosa vitambulisho vya kitaifa. Bila kitambulisho, huwezi kutibiwa katika hospitali ya serikali, watoto wako hawawezi kunufaika kutokana na elimu bila malipo, huwezi ukajisajili kupata cheti cha usafiri au leseni ya gari. Huwezi ukagombea kiti chochote cha kisiasa, kufungua akaunti ya benki au kusajili nambari ya simu. Hii ni kwa sababu hautambuliwi kikatiba kama kabila,” Aggrey Anyamba, mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 56, alieleza vyombo vya habari Kigumba.

“Watoto wetu hawajaweza kuendeleza elimu yao katika taasisi za juu za masomo kwa sababu kabila letu halitambuliwi. Hatuna siku za usoni. Ikiwa unamiliki kipande cha ardhi huwezi kukikodisha,” anaeleza Anyamba.

Jacob Kato, 43, ambaye ni mkulima anasema: “Hatuwezi tukaanzisha biashara hapa kwa sababu hatuna vitambulisho. Hii inamaanisha pia hatuwezi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.”

Edisa Namaji, 50, anaeleza kuwa Wamaragoli hupitia aina kadhaa za ubaguzi ikiwemo kuachwa na waume wao kutoka makabila mengine.

“Mwanamke Mmaragoli anapoolewa na mwanamme nje ya kabila lake hastahili kama mke. Wanaume kutoka makabila mbalimbali huwa wanatuacha. Kwa mfano, mume wangu kutoka kabila la Acholi aliniacha na sasa ninateseka na watoto wetu. Alioa mwanamke wa kabila lake kutoka Wilaya ya Gulu,” mama huyo wa watoto watano analalamika.

“Siwezi kuwasajilisha watoto wangu kupata vitambulisho kwa sababu sitambuliwi. Ikiwa nitatambuliwa kikatiba, nitakuwa na sauti ya kuzungumza kuhusu matumaini na changamoto zangu,” anasema.

Mipango ya Serikali

Serikali imetangaza mipango ya kubuni tume ya kufanyia katiba marekebisho itakayoangazia malengo yaliyowasilishwa katika mswada wa mwanachama wa siri unaokusudia kubadilisha usimamizi wa Benki Kuu, kutambua jamii ya Maragoli na kuhakikisha usambazaji sawa wa nafasi za ajira.

Serikali ilikuwa imeweka muda wa kubuni tume hiyo hiyo kabla ya mwisho wa Bunge la 10, mnamo Mei 2021.

Kulingana na MRG, chimbuko la wanajamii wa Maragoli Uganda halijarekodiwa kwa kina katika vitabu vya kihistoria.

MRG inasema kuwa Wamaragoli huenda walitoka Uhabeshi kupitia Kusini mwa Sudan kuelekea eneo la kusini mwa Mto Nile Magharibi na maeneo ya Bunyoro.

Hata hivyo, Christopher Kagunza, mwenyekiti wa Muungano wa Jamii ya Maragoli anasema: “Tulihama kutoka Saudi Arabia katika Karne ya 18 ambapo baadhi wetu tulianza kuishi Hoima wengine Masindi, Kigumba na Bugiri. Kundi la mwisho lilienda kuishi Magharibi mwa Kenya.”

Anaeleza kuwa mnamo 1903, baadhi ya Wamaragoli wenye ujuzi kutoka Kenya walisajiliwa kufanya kazi kwenye reli ya Uganda na baadaye wakaanza kuishi Kigumba.

“Katika miaka ya 1920, serikali ya Uingereza katika Mpango wa Maendeleo Uganda iliingia kwenye mkataba na Ufalme wa Bunyoro Kitara kuwapa makao Wamaragoli kutoka Kenya eneo la Bunyoro. Hii ni baada ya Omukama (Mfalme) Bw Tito Winyi IV Gafabusa wa Bunyoro Kitara (1924 – 1967) kushuhudia uwezo wetu katika kilimo. Aliwatambua Wamaragoli kama wakulima bora wa mahindi, pamba, maharagwe, mihogo na mtama katika ufalme wake,” alifafanua Kagunza.

Moses Sagwa, mkulima mwenye umri wa miaka 50 na mhubiri, anasema kuwa kundi la 1920 lilikuja na Biblia na likasambaza injili eneo hilo.

“Wengi wetu ni wa Pentekosti na wakulima eneo hili. Tulikubaliwa hapa kwa sababu ya ujirani na undugu wetu mwema,” anasema Sagwa.

Anyamba anaeleza kuwa jamii ya Maragoli imechangia pakubwa katika kilimo jambo ambalo limesababisha maendeleo na ukuaji wa miji kama Kigumba.

“Tumeshiriki maendeleo ya kitaifa kijamii na kiuchumi kama vile kulipa ushuru na shughuli nyinginezo za kitaifa,” anaeleza.

Hata hivyo, Anyamba anafichua kuwa kwa sababu ya unyanyapaa na ubaguzi, baadhi ya watu hasa vijana hawataki kutambulishwa kama Wamaragoli.

“Binti zangu watatu walilazimika kuchukua majina ya Kinyoro ili wajiunge na shule ya msingi. Kutambuliwa na Katiba kutatukomboa. Hakuna yeyote atakayekuwa akiwadunisha Wamaragoli kwa sababu tutakuwa sote sawa katika kikatiba. Tutakuwa huru kutokana na aina yoyote ya kuingizwa baridi na tutaweza kupata huduma zote za kitaifa,” anasema Kagunza.

Kwa upande wake Sagwa, anahoji kuwa “Watoto wetu wataweza kupata elimu na ufadhili wa masomo. Tutaweza kukodisha ardhi yetu na kuwania nyadhifa za uongozi nchini.”

Mila na tamaduni

Wamaragoli, wanaozungumza lugha inayofahamika kama Lugoli, zamani walikuwa wakishiriki ndoa za wake wengi na urithi wa wajane lakini mila hizo sasa zimebadilika.

“Tumekuwa tukishiriki ndoa za wake wengi na urithi wa wajane lakini janga la HIV/Aids pamoja na gharama ya juu ya maisha imepunguza tamaduni hizo kwa njia nyingi,” anafafanua Mzee wa jamii ya Maragoli Luka Mudolya.

Katibu wa Muungano wa Jamii ya Maragoli, David Ndoli, anasema kuwa jamii yake bado inashiriki utamaduni wa kuwapasha tohara wavulana unaofahamika kama kekebo kwa Lugoli.

“Bado huwa tunawatahirisha wavulana na tambiko hilo ni nguzo ya utamaduni wetu na huambatana na ngoma na tamaduni nyinginezo,” anaeleza.

Kuhusu suala la kuwatambua Wamaragoli kikatiba, meneja wa MRG Afrika jijini Kampala, Agnes Kabajuni, anasema hatua hiyo itawasaidia wanajamii hao kupata tena utambulisho na hadhi yao katika jamii.

“Itaimarisha uraia wao kama watu walio kwenye hatari ya kukosa taifa. Wataweza kupata stakabadhi za kisheria kama vile vitambulisho na pasipoti si kama makabila mengine, lakini katika kundi lao binafsi. Stakabadhi halali pia zinahusishwa na kupata huduma, elimu na ajira. Itasaidia serikali kutimiza wajibu wake kitaifa wa kuangamiza hatari ya kuishi bila taifa Uganda,” anaeleza Kabajuni.

Kuhusu iwapo ingekuwa bora kutambua makabila yote ya walio wachache nchini Uganda katika marekebisho hayo ya katiba mara moja badala ya kabila moja baada ya lingine, Kabajuni anafafanua: “Ingekuwa vyema kuwa na mswada mmoja. Nafasi ya kuwa na Mswada kuhusu kujumuisha jamii za wenyeji unapaswa kuisadia serikali kuzingatia jamii nyinginezo ambazo hazipo katika Awamu ya Tatu ya Katiba.”

Japo Uganda ina makabila 21 na idadi ya watu milioni tatu, Wakfu wa Tamaduni Mseto Uganda (CCFU) unahoji kuwa huwa hayajumuishwi katika mijadala yoyote ya kisiasa au kitamaduni.

Baadhi ya makabila mengine ya makaundi ya walio wachache Uganda ni pamoja na Babukusu, Babwisi, Bamba, Banyabindi, Basongora, Kebu, Lendu, Nubi, na Paluo (almaarufu kama Chope), Tepeth, Banyara, Batuku, Batwa, Dodoth, Mening, Jie, Mvuba, Nyangia, Bagwe, Bagungu, Bakenyi, Ngikutio, Basese, na Bagangaizi.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Rais Suluhu ametoa ishara...

WANDERI KAMAU: Uchaguzi ujao utumiwe kulainisha siasa zetu