Wambora ailaumu Serikali kwa kudhalilisha wakulima

Wambora ailaumu Serikali kwa kudhalilisha wakulima

NA RICHARD MAOSI

BARAZA la Magavana (CoG), Wizara ya Kilimo, Shirika la Kutoa Msaada Duniani (USAID) ziliandaa mkutano mjini Naivasha kujadili matatizo yanayokumba wakulima wa kahawa na chai nchini.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora, walikubaliana kuwa pana haja ya kuleta ushirikiano, baina ya wawekezaji wa kibinafsi na serikali.

Wambora alilaumu Wizara ya Kilimo, kwa kupitisha sheria ambazo hazikuwa zikimlinda mkulima wa kawaida, kama vile kodi ambazo zinaumiza wakulima.

“Wizara ya Kilimo imekuwa ikipuuza jukumu la serikali za kaunti, hivyo basi tutashirikisha Bunge na Seneti kupinga baadhi ya miswada ambayo inanyanyasa wakulima,”akasema.

AlIeleza kuwa The Tea Act 2020 ambayo ilipitishwa tarehe 21Januari 2021, iliyotolewa na wizara kudhibiti sekta ya majani chai ni kinyume na katiba, kwani serikali za kaunti hazikushirikishwa.

Hata hivyo alisema kuwa mageuzi katika sekta ya kahawa yanalenga kunufaisha mkulima wa kawaida , na ndio maana magavana kutoka kaunti mbalimbali wameamua kushirikiana ili kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa ifikapo Machi.

“Leo hii tumekubaliana kwa kauli moja kuwa tutatumia utaratibu kupinga baadhi ya mawazo ambayo yanaelekea kukinzana na majukumu ya Kaunti, kilimo ikiwa ni mojawapo,”alisema.

Wambora alisema kuwa utendakazi wa kilimo unapatikana katika serikali za ugatuzi, hivyo basi serikali haikuwa na nafasi ya kuingilia kati.

Pili alipendekeza kuwa magavana wanatafuta muda wa kujadiliana na rais Uhuru Kenyatta , ili kurekebisha Tea Act 2020, ambayo inawakandamiza wakulima wa majani chai.

Aidha aliomba wizara ya Fedha kutoa hela mapema ili kufanikisha miradi kwa wakati mashinani kwa wakulima ambao wanategemea kilimo.

Alilaumu serikali ya kitaifa kwa kuchukua muda mrefu, kugharamia miradi ya wakulima, kwa sababu hela zilizokuwa zikifika mashinani sio za kutosha.

Aidha alishtumu serikali kuu kwa kwenda mwendo wa kinyonga wakati wa kukabiliana na nzige ambao wamekuwa wakiharibu mimea ya wakulima na kukwamisha shughuli za kilimo.

You can share this post!

Mazishi yageuka rungu la kuchapa Ruto

Sonko kuendelea kukaa hospitalini