Habari Mseto

Wambora alivyoponea tena mahakamani

August 17th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MATUMAINI ya aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Livuti  kuwa Gavana wa kaunti hiyo yalitokomea Ijumaa baada ya Mahakama ya Rufaa kuhalalisha ushindi wa Bw Martin Wambora.

Uamuzi huo wa mahakama hiyo umemfanya Bw Wambora kupumua akijua sasa atakamilisha kipindi cha miaka mingine mitano akiwa kileleni cha uongozi wa kaunti ya Embu.

Kubatilishwa kwa uamuzi wa mahakama kuu iliyofutilia mbali ushindi wa Bw Wambora kumethibitisha bayana kwamba mawimbi ya kisiasa yanayompiga Bw Wambora hayamtigishi kisiasa.

Wakati wa kipindi cha kwanza cha uongozi wake Bw Wambora alipona majaribio mawili ya kuondolewa mamlakani kupitia hoja iliyowasilishwa na Bw Kivuti.

Baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Agosti 6 2017 , Bw Kivuti aliwasilisha kesi ya kupinga matokeo.

Wakitoa uamuzi katika kesi ya Gavana Wambora, Majaji William Ouko, Daniel Musinga na Fatuma Sichale walisema , “mshtakiwa hakufanya chochote kinachoweza kufanya ushindi wake ubatilishwe.”

Walifutilia mbali uamuzi wa Jaji William Musyoka aliyesema kuwa Gavana Wambora hakushinda kwa njia halali.

Bw Wambora alimshinda Bw Kivuti wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Bw Kivuti aliwasilisha kesi kupinga ushindi huo akimlaumu mpinzani wake kwa kushirikiana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kukaidi sheria za uchaguzi katika hari yake ya kuhifadhi kiti hicho.

Wakithibitisha kuwa Bw Wambora alimshinda Bw Kivuti kwa njia halali, majaji hao walisema Gavana huyo hakufanya makosa yoyote kama alivyodai mpinzani wake.

“Makosa ambayo Wambora alilimbikiziwa hayatokani naye mbali ni maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) walioyatenda,” walisema majaji hao.

Mahakama ilisema makosa ambayo Bw Kivuti alimwelekea Bw Wambora hayana msingi.

Baada ya kusema hayo majaji hao walisema kuwa Bw Wambora hapasi kubeba msalaba usiokuwa wake.

Walisema makosa yaliyotokana na uchaguzi  huo kamwe “hayawezi kuwekelewa Bw Wambora.”

“Bw Kivuti ambaye alimshtaki Gavana Wambora hakuwasilisha ushahidi ambao korti ingeutegemea kuvuruga matokeo ya uchaguzi. Mahakama kuu ilipotoka kufikia uamuzi kwamba Bw Wambora alishinda kwa njia isiyofaa,” walisema majaji hao.

Majaji Ouko, Musinga na Sichale walisema kuwa mahakama kuu ilitegemea ushahidi ambao haukuwasilishwa kortini  kuharamisha

Mnamo Februari, mahakama kuu ya Embu ilifutilia mbali ushindi wa Bw Wambora na kusema zoezi la uchaguzi lilikumbwa na kasoro nyingi na ukiukaji usio na kifani wa sheria za uchaguzi.

Jaji Musyoka alisema katika uamuzi wake kuwa makosa mengi yaliguduliwa katika stakabadhi za uchaguzi na “kutilia shaka ushindi wa Bw Wambora.”

Jaji Musyoka alisema hesabu ya kura alizopata Bw Wambora ilikuwa imeborongwa.

Alisema kuwa Fomu 37A zilizokuwa zimejazwa matokeo zilikuwa hazimo huku nyingi ya zile zilizokuwapo zikikosa kusomeka.

Alisema kura zilipohesabiwa tena mahakamani iliguduliwa kuwa kulikuwa kura 111 za ziada ambazo hazikuwa za aidha Bw Wambora ama Bw Kivuti.

Jaji Musyoka alikubaliana na Bw Kivuti kuwa huenda kura hizo ziliwasilishwa pale kinyume cha sheria kuvuruga matokeo ya uchaguzi huo.

Bw Kivuti aliwania kiti cha kaunti ya Embu kwa tikiti ya chama cha Maendeleo Chap Chap chake Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua.

Tofauti kati ya ushindi wa Bw Wambora’s  na Bw Kivuti ulikuwa kati ya kura 700 na 800.

Jaji Musyoka Fomu 37A ambazo hazikusomeka ziliathiri matokeo ya kura 10,000.

Na wakati huo huo majaji hao hao walihidhinisha ushindi wa Mbunge wa Starehe Bw Charles Njuguna almaarufu Jaguar.

Uhsindi wake ulikuwa umepingwa na mwaniaji wa kiti hicho wa  Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Steve Mbogo.