Habari MsetoSiasa

Wambora ashtaki madiwani kwa kuzuia ukusanyaji ushuru

November 11th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

GAVANA wa Embu Martin Wambora, ameshtaki Bunge la Kaunti kwa kupitisha hoja ya kusimamisha shughuli ya ukusanyaji ushuru.

Gavana anataka Mahakama Kuu ya Embu kufutilia mbali uamuzi wa Bunge la Kaunti hiyo.

Madiwani walipitisha hoja hiyo kama njia mojawapo ya kumshinikiza gavana huyo kuwasimamisha kazi maafisa wanaodaiwa kuhusika na ufisadi katika serikali ya kaunti.

Gavana aliitaka mahakama kutaja kesi hiyo kuwa ya dharura.

Bw Wambora ameshtaki Bunge la Kaunti, Spika Josiah Thiriku na Karani Jim Kauma.

Katika uamuzi wake, Jaji Flurence Muchemi aliagiza Katibu wa Kaunti ya Embu, Bw Jason Nyaga kutotekeleza uamuzi wa Bunge la Kaunti hadi pale kesi hiyo itasikilizwa na kuamuliwa.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 14, mwaka huu.

Katika kesi yake, Bw Wambora anasema kuwa uamuzi wa bunge hilo la kaunti utatiza shughuli za serikali ya kaunti.

Hoja hiyo ilikuwa imefadhiliwa na Kiongozi wa Wachache, Bw Newton Kariuki aliyetaka serikali ya kaunti kusitisha shughuli ya kuacha kukusanya ushuru kutoka kwa wafanyabiashara hadi gavana atakaposimamisha kazi maafisa wafisadi.