Habari za Kitaifa

Wambora, Waititu sasa Kawira: Kaunti za Mlima Kenya zatawaliwa na uchu wa kutimua magavana


HOJA ya kumuondoa mamlakani Gavana wa Meru Kawira Mwangaza kwa mara ya tatu chini ya miaka miwili inafichua hali ngumu ambayo magavana wa eneo la Mlima Kenya wanapitia.

Uchambuzi wa hoja za kuwatimua magavana unaonyesha kuwa Mlima Kenya umeandikisha hoja nyingi zaidi za kuwatimua magavana tangu ugatuzi ulipoanza nchini mwaka wa 2013.

Kaunti 10 za eneo pana la Mlima Kenya pia zimekuwa na magavana wengi katika chaguzi kuu tatu zilizopita, huku Kiambu ikiwa na gavana wa nne, Kimani Wamatangi aliyetanguliwa na William Kabogo, Ferdinand Waititu na David Nyoro.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017 wapigakura katika eneo la Mlima Kenya waliwatimua karibu magavana wote waanzilishi isipokuwa aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria na aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora.

Hii ni tofauti na maeneo mengine ya nchi ambapo magavana wengi wamehudumu kwa mihula miwili.

Kufikia sasa, jumla ya magavana 11 na manaibu watatu wametimuliwa na madiwani tangu 2013, lakini ni magavana wawili tu – aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Bw Waititu (Kiambu), na naibu gavana wa Kisii Robert Monda – walioondolewa afisini, huku wengine wakiokolewa na seneti na mahakama.

Mabunge ya kaunti yamepiga kura kupitisha kuondolewa afisini kwa Bi Mwangaza (mara tatu), Bw Mwangi wa Iria, Bw Granton Samboja (aliyekuwa gavana wa Taita Taveta), Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Bw Paul Chepkwony (aliyekuwa gavana wa Kericho) na marehemu Gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua, lakini waliokolewa na Seneti.

Aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora na mwenzake aliyekuwa wa Wajir Mohamed Abdi pia walitimuliwa afisini na madiwani na kuondolewa kwao kukaungwa mkono na maseneta.

Hata hivyo, walirejea afisini baada ya kuondolewa kwao kubatilishwa na mahakama.Bw Wambora alikuwa gavana wa kwanza 2014 kuondolewa mamlakani.

Gavana huyo, ambaye baadaye alimaliza mihula miwili, aliondolewa mamlakani mara nne mwaka wa 2014.Februari 2014, madiwani wa kaunti walipiga kura ya kumwondoa afisini, lakini Mahakama Kuu ilibatilisha hatua hiyo kwa msingi kwamba mahakama ilikuwa imesitisha mchakato huo.

Aprili, walimshtaki tena na uamuzi wa bunge hilo ukaidhinishwa na Seneti baada ya maseneta 40 kupiga kura ya kuunga mkono.

Lakini Majaji wa Mahakama ya Rufaa; GBM Kariuki, John Mwera na Hannah Okwengu waliubatilisha uamuzi huo kwa ukosefu wa ushahidi kwamba alikiuka katiba, na hivyo kumpa nafasi ya kuhudumu mihula miwili kama gavana.

Naibu Gavana wa Siaya William Oduol na aliyekuwa naibu gavana wa Machakos Bernard Muia Kiala pia waliondolewa na madiwani lakini wakaokolewa na seneti.

Bw Monda, hata hivyo, hakuwa na bahati baada ya seneti kuunga mkono kuondolewa kwake.