Michezo

Wambua, Odera mstari wa mbele kupokezwa mikoba Shujaa

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KEVIN Wambua na Paul Odera ni miongoni mwa wakufunzi wanaopigiwa upatu wa kupokezwa mikoba ya timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) limesema linaelekea kukamilisha mchakato wa kutafuta kocha mpya wa Shujaa kwa minajili ya duru zilizosalia za raga ya dunia msimu huu.

KRU ilikatiza uhusiano na mkufunzi Paul Feeney aliyevunja rasmi ndoa kati yake na shirikisho hilo mwishoni mwa Aprili 2020 na kurejea kwao New Zealand baada ya kuongoza Shujaa kutia kibindoni ubingwa wa Raga ya Afrika.

Ushindi huo uliwakatia Shujaa tiketi ya kufuzu kushiriki makala ya 32 ya Michezo ya Olimpiki yatakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2021 baada ya kuahirishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi kutokana na janga la corona.

Feeney aliyewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Fiji mnamo 2015, pia aliiongoza Kenya Morans kutinga fainali ya Tusker Safari Sevens mnamo 2019 japo alishindwa kuongoza Shujaa kukamilisha duru za Raga ya Dunia zilizositishwa kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.

Shujaa wanatazamiwa kurejea ulingoni kunogesha duru nne za mwisho za Raga ya Dunia msimu huu jijini London na Paris mnamo Septemba kabla ya kutua Singapore na Hong Kong mnamo Oktoba, 2020.

Feeney aliondoka Kenya kuelekea New Zealand kujumuika na familia yake baada ya kushikilia mikoba ya Shujaa na Morans kwa kipindi kifupi.

“KRU ingependa kumshukuru Feeney kwa mchango wake katika makuzi ya raga yetu kwa kipindi alichohudumia timu ya taifa. Tunamtakia kila la heri katika shughuli zake za baadaye,” ikaongeza taarifa hiyo.

Feeney aliteuliwa kuwa kocha wa Shujaa mnamo Septemba 2019 baada ya mkataba wa Paul Murunga kutamatika. Wambua ambaye kwa sasa anawanoa pia Kenya Lionesses, aliteuliwa msaidizi wake.

Chini yake, Kenya Morans walinyakua ufalme wa Safari Sevens mnamo 2019 huku Shujaa wakiridhika na nishani ya shaba katika mashindano hayo yaliyonogeshwa pia na Ufaransa, Afrika Kusini, Amerika, Uhispania, Ureno, Namibia na Hong Kong.

Ingawa hivyo, matokeo ya Shujaa katika Raga ya Dunia hayajakuwa ya kuridhisha zaidi chini ya Feeney hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa wanashikilia nafasi ya 12 kwa alama 35 baada ya kutandaza duru sita katika kivumbi hicho cha duru 10.

Feeney amewahi pia kunoa vikosi vya raga vya Auckland na Stormers nchini New Zealand na Afrika Kusini mtawalia. Odera kwa sasa anadhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Simbas na kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu.