HabariSiasa

Wameingia 'box' ya Jubilee?

April 8th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetangula wameonekana kumezwa na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kama Raila Odinga alivyomezwa.

Wiki iliyopita, wawili hao pamoja na Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, walishirikiana na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuzindua usajili wa watu kidijitali na pia wakahudhuria hotuba ya rais bungeni.

Uwezekano kuwa hata Bw Mudavadi ameamua kufanya kazi na serikali umezua mjadala kuhusu kumalizwa kabisa kwa upinzani nchini.

Bw Mudavadi amekuwa akionekana kuwa mtu pekee aliyeweza kupuuza ushawishi wa Serikali na ndiye amekuwa sauti mpya ya kukosoa serikali.

Hii ni baada ya Bw Odinga kubadili msimamo na akakoma kukosoa serikali, na badala yake kuiunga mkono katika kila suala, kinyume na awali ambapo alikuwa sauti ya mwananchi.

Bw Kalonzo naye alitangaza mwaka jana kuwa atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Kenyatta huku Bw Wetangula akibakia kimya.

Lakini bw Mudavadi amekanusha kuwa amemezwa na Serikali: “Sijamezwa. Kilichopo ni kuheshimu ustaarabu wa Rais kutualika kila mmoja kibinafsi katika shughuli hizo mbili za kitaifa.”

Baada ya hotuba ya Rais Kenyatta kwa Bunge mnamo Alhamisi, Bw Mudavadi ndiye pekee aliyemkosoa kwa kukosa kuwaondoa mawaziri wanaochunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Mabwana Odinga, Musyoka na Wetangula kwa upande wao walimpa Rais sifa kochokocho kwa hotuba yake, ambayo ilipuuza masuala muhimu zaidi kwa wananchi kama vile gharama ya juu ya maisha na njaa.

Kwa upande wake, Bw Wetangula yanayoshuhudiwa ni matukio ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa taifa haliwezi kutawaliwa kwa handisheki, mbali kinachohitajika ni sera zinazokubalika na wote.

Lakini kulingana na Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing, kuhusika kwa wawili hao kwenye shughuli za kiserikali ni mbinu ya kisiasa.

“Hatua ya Kalonzo, Mudavadi na Wetangula kuanza kumkaribia Raila ni ishara wazi kuwa kinara wao anaondoka kwenye siasa. Kama fisi anavyofuata mtu akidhani mkono utaanguka aukule, hata hao wanafanya hivyo wakitarajia kunufaika Raila akiondoka,” akasema Bw Pkosing.

Alieleza kuwa mbinu nyingine ni kuwa wanasiasa hao wanataka kukaa karibu na Rais, kwa matumaini kuwa atawaunga mkono kuwania urais 2022.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Macharia Munene anasema kuwa uhusiano wa majuzi kati ya Rais Kenyatta na vinara wa upinzani ni jambo ambalo limepangwa vizuri.

Naye Prof Peter Kagwanja anasema kuwa hatua hiyo ni matunda ya handisheki: “Ni dhihirisho kuwa mbinu ya Rais ya kuleta umoja nchini inafanikiwa. Rais amelipatia suala la umoja umuhimu mkubwa katika utawala wake.”

Kwa upande mwingine, hatua ya wakuu wa upinzani kukaribia Rais Kenyatta imezua upinzani kutoka kwa mrengo wa Naibu Rais William Ruto, ambao wanaiona kama yenye lengo la kumtenga zaidi tangu.

Dkt Ruto alikosa kushiriki uzinduzi wa usajili wa kidijitali kutokana na kile wadadisi wanasema ilikuwa kuonyesha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Rais Kenyatta kuwashirikisha vinara wa upinzani.