Bambika

Wamekwepa skendo na drama licha ya kuweka penzi hadharani

April 5th, 2024 3 min read

NA SINDA MATIKO

UNAPOKUWA staa tena uwe kwenye mahusiano, ni vigumu sana kuepuka mahusiano yako kupigwa msasa.

Mapaparazi siku zote hukesha kuwafuatilia wakiwa tayari kuanika habari zozote zinazohusiana na mahusiano yao.

Mara nyingi habari ambazo hutrendi huwa ni zile mbaya hasa pale mahusiano ya mastaa yanapoingia nyongo na kuibua madrama.

Kwa mfano, ndoa ya DJ Mo na mkewe Size 8, haipiti mwaka bila ya drama.

Jambo hili limewafanya mastaa wengi kujitahidi kuwa sio tu makini na mahusiano yao lakini pia kuyafaya kuwa siri ili kuhakikisha wanazikwepa skendo za aina yoyote ile.

Hata hivyo, kuna kundi moja la mastaa ambalo limefanikiwa kuendelea kuanika mapenzi yao hadharani bila ya kuhusishwa na skendo wala drama za aina yoyote ile.

Wakati wenzao wakihangaika na tetesi za kila kukicha na drama za hapa na pale, kapo hizi zimekuwa zikidumisha picha ya kuwa kila kitu kwao kipo sawa.

Hii ina maana kuwa hata pale kapo hizo zinapogombana au kuwa na mtafaruku, hadhira na mashabiki wao hasa wa mitandaoni huwa hawapati picha hiyo.

Hizi hapa kapo hizo zisizofahamika kwa kuhusishwa na drama katika mahusiano yao.

AMINA ABDI NA DJ JOHN RABAR

Mtangazaji huyo alianza mahusiano ya kimapenzi na DJ John Rabar, mmoja wa waasisi wa Homeboyz Radio, alipokuwa akifanya kazi kwenye kituo hicho.

Mahusiano yao yaliishia kwenye ndoa 2012. Kwa miaka 10 ya ndoa yao, hapajawahi kutokea drama au skendo kwenye uhusiano wao.

Amina na Rabar pamoja na uhusiano wao kujulikana na umma, ni kapo moja yeye usiri sana kuhusu maisha yao.

Tofauti na kapo zingine, zinapatikana picha chache sana za Amina na Rabar mitandaoni.

Mara ya mwisho penzi lao kugonga vichwa vya habari ilikuwa 2021 Amina alipompiga sapraizi mumewe kwa kumnunulia Play Station 5 (PS5) kwenye bathidei yake.

ZIA BETT NA NYASHINSKI

Baada ya kuwa wapenzi kwa kipindi kirefu, hatimaye kapo hii ya msanii na bloga ilifunga harusi Disemba 10, 2021.

Ilikuwa ni sherehe ya kimya kimya sana huku waalikwa wakiwa ni watu wao wa karibu hasa maceleb.

Kapo hii ambayo ilianza kudeti 2017 kabla ya kuja kufunga ndoa, imefanikiwa pakubwa kubania mashabiki wao kujua mengi kuhusu ndoa yao.

Ni ndoa ambayo haijawahi kukumbwa na drama.

ESTHER MUSILA NA GUARDIAN ANGEL

Ndoa ya mastaa hawa inaingia mwaka wa pili sasa. Penzi lao liliposhika nare, 2020, liliangaziwa kweli kweli na mapaparazi ishu kubwa ikiwa ni tofauti kubwa ya umri kati ya Bi Musila 54 na Guardian 33.

Kando na tofauti kubwa kiumri kati yao, hakuna kingine kilichowahi kuripotiwa pakubwa kuhusu ndoa yao. Haijawahi kuibuka drama wala skendo ndani ya ndoa hiyo huku wawili hao siku zote wakiishia kusifiana hadharani.

Japo Musila na Guardian huwa hawafichi sana penzi lao wakionekana hadharani mara kwa mara, mengi ya ndani kuwahusu husalia nao.

SERAH TESHNA NA VICTOR WANYAMA

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Harambe Stars, anajulikana kwa kupenda kuishi maisha ya usiri.

Taarifa nyingi za penzi lao zimekuwa zikiibuliwa na Serah ambaye alithibitisha kuwa kwenye mahusiano na staa huyo mwaka jana.

Kilichowaacha wengi vinywa wazi ni pale Serah alipofichua kwamba penzi lao lilikuwa limedumu kwa miaka saba kabla yao kuja kuyaweka hadharani.

Hata ujauzito, Serah aliuweka kuwa siri kubwa hadi alipofichua mwenyewe. Kama kuna kapo ambayo ni ngumu kupata taarifa zao pasi na wao kuzitoa basi itakuwa ni hii.

JOYCE OMONDI NA WAHIGA MWAURA

Uhusiano kati ya mwanamuziki wa injili Joyce na mume wake mwanahabari wa BBC Mwaura, ulipata kujulikana hadharani Disemba 2015 walipofunga ndoa.

Mwaka jana, kapo hiyo ilisherehekea kutimiza miaka minane ya ndoa yao. Kumekuwa na jitihada za mapaparazi kulifuatilia penzi lao kwa lengo la kuwachomea lakini mara nyingi taarifa zimekuwa zikikosekana.

Kapo hii imefanikiwa kudumisha ndoa yao kwa miaka yote hiyo pasi na kuhusishwa na drama yoyote ile. Joyce aliwahi kukiri kuwa siri iliyodumisha ndoa yao na kuiepusha na drama ni “kufanya mambo yao kimya kimya.”

“Siri ya wazi ni kwamba nimeolewa, ila siri ya kudumisha ndoa yetu ni kufanya mambo yetu kimya kimya maana nilipofunga ndoa niliolewa na Waihiga pekee na wala sio jamii au watu wengine,” aliwahi kusema Joyce.

NANA OWITI NA KING KAKA

Mahusiano yao yaliwahi kuwa na msukosumo zaidi ya miaka 10 iliyopita King Kaka alipomchepukia Nana na mwanamuziki Sage Chemutai.

Lakini baada ya kuomba msamaha na kubadilisha mienendo, kapo hii imeishi maisha ya kusifiana hadharani kiasi kwamba imekuwa vigumu kwa mapaparazi kupata taarifa zozote za uwepo wa mtafaruku kwenye ndoa yao.

JUDY NYAWIRA NA ABEL MUTUA

Ni kama vile kapo hii huwa haipitii msukosuko kwenye ndoa yao. Kwa miaka 15 sasa toka wafunge ndoa, hamna drama au skendo iliyowahi kuikuta kapo hii. Mara si moja Abel amekuwa akisikika akikiri kuwa kama sio uwepo wa mkewe, maisha yake yangelikuwa tofauti.

LULU HASSAN NA RASHID ABDALLA

Wanandoa hawa wanahabari wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 15 na hakujawahi kutokea drama kwenye ndoa yao licha ya mahusiano yao kuwa wazi sana ukiongezea umaarufu.

Hii ni licha ya kufanya shughuli zao nyingi kwa pamoja ikiwemo kusoma habari na uendeshaji wa kampuni yao ya filamu Jiffy Pictures.

NAMELESS NA WAHU

Ndio kapo kongwe ya mastaa iliyoweza kudumisha penzi na ndoa yao bila ya kuwepo na drama.

Ndoa yao ina miaka 20 sasa na haijawahi kutokea drama au msukusuko japo hadharani.