Wamiliki hoteli waelezea hofu kuhusu Covid-19

Wamiliki hoteli waelezea hofu kuhusu Covid-19

KALUME KAZUNGU NA WINNIE ATIENO

Wafanyabiashara katika sekta ya utalii ukanda wa Pwani, wamehakikishia watalii nchini na kimataifa watakuwa salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, huku serikali ikianza kurudisha kanuni za kuepusha maambukizi hayo yanayoongezeka.

Wafanyabiashara hao wameibua hisia mseto kuhusu athari za ongezeko la maambukizi hayo kwa sekta ya utalii.

Maambukizi hayo yalisababisha serikali kurudisha baadhi ya kanuni zilizokuwa zimelegezwa kama vile hitaji la kuvalia barakoa katika maeneo ya watu kukongamana.

Baadhi ya wadau wa utalii wameeleza wasiwasi kwamba, hali hii huenda ikaibua tena athari mbaya kwa biashara zao, huku wengine wakisema walikuwa washajiandaa vilivyo katika miaka miwili iliyopita kuepusha maambukizi katika biashara zao na hivyo wanaamini wateja hawatakuwa na wasiwasi kuendelea kutalii Kenya.

Wadau mbalimbali waliohojiwa na Taifa Leo wamewataka Wakenya kudumisha kanuni za kuepusha maambukizi zaidi ya Covid-19.

Mnamo Jumatano, Wizara ya Afya ilitangaza maambukizi mapya kitaifa ndani ya saa 24 zilizopita ambapo yalikuwa 419, Pwani kukiwa na visa 20.

“Sisi hatukulegeza kamba licha ya kupungua kwa virusi na maambukizi nchini. Isitoshe, tuna sera kali katika maeneo yetu ya biashara zinazohitaji kila mteja kuvalia barakoa. Kwa hivyo kama sekta, sisi hatuna wasiwasi maanake pia wafanyakazi wote hupokea chanjo,” akasema Mwenyekiti wa Muungano wa Wahudumu wa hoteli, Dkt Sam Ikwaye.

Hata hivyo, wadau wengine walisema tangazo la serikali kuhitaji watu kuvalia barakoa katika sehemu za makongamano linaibua taswira kwamba kuna hatari nchini.Kwa msingi huo, wanaamini kanuni za kudhibiti virusi vya corona zilizorejeshwa huenda zikaathiri biashara zao.

“Watalii wanahisi hawako salama. Wengi sasa wanaogopa kujivinjari kwa kuhofia kuambukizwa corona,” akasema mmiliki wa hoteli kisiwani Lamu, Bw Abdallah Ali.

Bw Mohamed Omar, anayetoa huduma ya kutembeza watalii ufuoni alisema, idadi ya watalii ilikuwa inaongezeka tangu kanuni za kudhibiti Covid-19 zilipolegezwa lakini sasa kuna wasiwasi.

“Wageni na wenyeji tayari walikuwa wamezoea kutembea bila maski. Ukimtangazia mtu leo hii kwamba lazima avalie barakoa, huwa anahisi hakuna usalama kiafya. Tunahofia tangazo la Waziri Kagwe litaathiri shughuli nyingi, hasa Pwani,” akasema Bw Omar.

Utalii ni mojawapo ya sekta muhimu ambazo ni uti wa mgongo kwa uchumi wa Pwani.

Sekta hiyo ni mojawapo ya zile zilizoathirika zaidi janga la virusi vya corona lilipotikisa ulimwengu 2020, lakini ikaanza kuinuka baada ya serikali kulegeza baadhi ya kanuni za kuepusha maambukizi wakati yalipokuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa kuwa athari kubwa ilisababishwa na vikwazo vya usafiri wa kimataifa, wadau wa utalii waliwekeza sana kwa mbinu za kuvutia watalii wa ndani ya nchi, mbali na maandalizi ya makongamano, mikutano na tamasha za aina mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

DARUBINI YA UKWELI: Ripoti ya TJRC inarejelea Vita vya...

Yego kuwinda tiketi ya dunia Omanyala akiahidi kutimka...

T L