Wamiliki hoteli wapinga ushuru wa vitanda

Wamiliki hoteli wapinga ushuru wa vitanda

Na WACHIRA MWANGI

WAMILIKI wa hoteli na wafanyabiashara kutoka Mombasa, Kwale na Kilifi wametoa wito kwa serikali za kaunti kuondoa ushuru wa vitanda, ipunguze leseni za kufanya biashara na pia ushuru wa pombe wakati huu sekta ya utalii inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi.

Mwanachama wa kamati kuu ya Muungano wa wafanyakazi na wahudumu hotelini (KAHC) Dkt Sam Ikwaye alisema serikali ya kaunti ya Mombasa inaendelea kuwaumiza kwa kutoza ushuru wa vitanda ilhali hawana wageni baada ya sekta ya utalii kuathirika kutokana na janga la virusi vya corona.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta afunge nchi kutokana na wimbi la kwanza la corona, kaunti hizo tatu zinazotegemea utalii, zimeathirika kimapato huku watalii wakipungua na kukabiliwa na mzigo mkubwa wa kuwalipa wafanyakazi wao na madeni wanayodaiwa na kampuni zinazowapa vyakula na huduma nyinginezo.

Dkt Ikwaye alisema hoteli chache zinazoendelea na biashara zimelemewa na haziwezi kumudu kuendelea na oparesheni zao chini ya sheria za kaunti.

“Inashangaza kwamba kaunti inasisitiza katika kutekeleza ushuru wa vitanda ilhali biashara zetu zinakabiliwa na wakati mgumu kutokana na uwepo wa corona,” akasema Dkt Ikwaye.

Afisa huyo sasa ametaka ushuru huo wa vitanda usitishwe. Pia wanataka ianze kutekeleza Hazina ya Fedha kwa wafanyakazi wa ufuoni ili wanachama waanze kuweka akiba kuwasaidia kukwamua biashara zao.

Mwenyekiti wa wamiliki wa baa katika Kaunti ya Kwale Richard Onsongo naye amemtaka Gavana Salim Mvurya kubuni mikakati ya kunusuru biashara zilizolemazwa na corona.

Bw Onsongo alisema kaunti hiyo hasa hutegemea watalii kutoka kaunti tano zilizofungwa na biashara zao zimeathirika kiasi kwamba hawawezi kuwalipa wafanyakazi wao. Alimtaka Bw Mvurya pia apunguze ushuru unaotozwa pombe kwa siku 60 ili biashara zao ziimarike kama zamani.

“Tunaomba miezi miwili au mitatu turuhusiwe kutolipa ushuru kwenye mauzo ya pombe kwa kaunti,” akasema Bw Onsongo.

You can share this post!

Mzozo mpya watokota Mumias Sugar

NASAHA ZA RAMADHAN: Tusipoteze fursa ya kutaka msamaha kwa...