Habari za Kitaifa

Wamiliki Matatu wasimamisha mgomo


MUUNGANO wa Wamiliki Matatu (MOA) umefutilia mbali mgomo uliopangiwa kufanyika kuanzia Agosti 26, 2024 ukisema serikali imekubali kujadiliana nao ili kusuluhisha masuala yanayozingira sekta hiyo ikiwemo kuhangaishwa na polisi.

Tangazo hilo ni afueni kuu kwa wazazi wanaopanga kuwarejesha watoto wao shuleni kwa muhula wa tatu.

Rais wa MOA, Albert Karakacha alisema Jumapili kuwa wanachama wake hawataondoa magari yao barabarani huku wakisaka suluhisho kwa changamoto zinazokabii sekta hiyo.

“Mgomo huo uliopaswa kufanyika umesitishwa. Tutashiriki mazungumzo na serikali kutatua masuala yanayoathiri sekta ya matatu,” alisema Bw Karakacha.

Alisema masuala yanayohusu kuhangaishwa na polisi ikiwemo serikali ya kaunti yameathiri oparesheni zao kote nchini.

Kama matakwa yao hayatafua dafu, muungano utatumia mbinu nyinginenzo ikiwemo kulemaza sekta ya usafiri nchini.

“Ni kuhusu kusimamisha, lakini ikiwa mazungumzo hayatajitokeza wazi wazi, itabidi tuketi pamoja na wanachama wetu na kubuni mwelekeo,”

Mgomo huo ulichochewa na uamuzi kutoka kwa Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA) kuweka kampuni ya Bima ya Invesco Assurance chini ya usimamizi wa mrasimu bila kuwapa muda wa kutosha kubadilisha mashirika yao ya bima.

“Sisi ni wafanyabiashara na tunashinikiza mgomo huu ufanyike kwa sababu ya masuala haya ambapo tumesakamwa mno na unaposukumwa, itabidi utafute namna ya kutetea uanachama wako.”

Hatua ya Mamlaka ya Nishati na Petroli (EPRA) ya kuongeza bei ya mafuta kutoka Sh18 hadi Sh25 kwa kila lita vilevile ni moja kati ya masuala yanayopingwa na sekta hiyo.

Taarifa ya Bw Karakacha imejiri siku chache tu baada ya usafiri kwenye barabara ya Ngong Road kutatizwa na matatu zinazotumia mkondo huo zikilalamikia kuhangaishwa na polisi.

Imejiri pia karibu wiki mbili baada ya kundi linalofahamika kama Matatu Move Kenya, linalowaleta pamoja viongozi wa vyama mbalimbali vya ushirika wa matatu jijini Nairobi, kuwasilisha malalamishi kuhusu kuhangaishwa na polisi wa trafiki.

Matatu Movement Kenya ilisema idadi kubwa ya wanachama wake waliokuwa wameandikisha magari yao na shirika la Invesco, walifumaniwa na polisi wamekuwa wakikamata magari yao bila kusikiza kilio chao.

Mwelekezi wa kundi hilo, Wambugu Kanoru, alisema hawana hiari ila kulemaza shughuli hadi serikali itakaposhughulikia malalamishi yao yanayoathiri sekta ya matatu.

Mwenyekiti wa muungano huo, Paul Thiongo alisema magari zaidi ya 1,000 yamepigwa mnada kufuatia agizo hilo la IRA kuhusu Invesco, iliyokosa kutimiza majukumu yake kifedha.