Habari Mseto

Wamiliki wa biashara ndogo hawatasazwa na KRA

November 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wamiliki wa biashara ndogo hawataponea baada ya serikali kuagiza Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) kuwafuatilia zaidi.

Serikali inataka KRA kuchunguza mashine za kunakili ushuru (ETR) ambazo hutumiwa na wafanyibiashara wadogo kwa lengo la kutambulisha wale ambao huwa hawalipi ushuru.

Hii ni kutokana na kuwa wafanyibiashara hao hukwepa kutumia mashine hizo baada ya kuuza bidhaa.

Mtambo wa ETR una uwezo wa kunakili kiasi cha bidhaa kilichouzwa, eneo zilikouzwa na wakati wa mauzo na kurahisishia KRA kujua kiasi cha ushuru kilicholipwa na mfanyibiashara.

“KRA inafaa kujitahidi kutambulisha wahalifu ambao hukwepa kulipa ushuru, wale wanaotumia mashine feki za ETR na kukataa kulipa VAT na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Rais Uhuru Kenyatta wakati wa kuadhimisha siku ya walipaji bora zaidi wa ushuru.