Habari Mseto

Wamiliki wa magari wahimizwa kuweka vidhibiti kasi

March 30th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAMILIKI wa magari ya uchukuzi wa umma wameshauriwa kukagua magari kabla ya kuruhusu yasafirishe abiria na mizigo barabarani.

Mwenyekiti wa chama cha kudhibiti usalama barabarani Road Safety Kenya Association, Bw David Njoroge Kiarie, alitaja ajali iliyotendeka majuzi eneo la Matuu Kaunti ya Machakos kama ya kusikitisha.

“Ninashuku dereva wa basi hilo la Medina Bus, lililotoka Wajir kuelekea Nairobi, kwamba alikuwa na uchovu mwingi na alikosa usingizi wa kutosha kwani ilikuwa majira ya saa kumi na moja za alfajiri,” alisema Bw Kiarie.

Alisema yule mtu anayestahili kupewa lawama zote ni mmiliki wa basi hilo ambaye alisema amekiuka sheria zinazohitaji kuweka kidhibiti kasi.

Akizungumza Ijumaa katika eneo ambapo ajali hiyo ilitokea Bw Kiarie aliwalaumu polisi wa Trafiki ambao alidai ni wengi kwenye barabara hiyo na hawawezi kushika hata basi moja lenye makosa.

“Ni jambo la kushangaza kupata ya kwamba kutoka mji wa Thika mpaka Matuu, kuna vizuizi vya trafiki 12 na bado kuna ajali mbaya zinazoshuhudiwa. Ningetaka serikali kuviondoa vizuizi hivyo iwapo havitekelezi umuhimu wowote.”

Alitaka polisi wa trafiki wafanye hima wamtie nguvuni mmiliki wa basi hilo la Medina kutoka Wajir kwa sababu yeye ndiye alikosa kuweka kithibiti mwendo katika gari lake.

Mkurugezi wa kampuni ya ukaguzi vifaa aina ya vidhibiti kasi nchini kwa jina Mvita Auto Diesel System Ltd, Bw Patrick Gakunga, alisema kulingana na uchunguzi wao ilibainika ya kwamba basi hilo lililohusika kwenye ajali lilikosa kidhibiti kasi.

“Tulishangaa kupata ya kwamba eneo la kidhibiti mwendo imefungwa kamba; jambo ambalo ni hatari kwa usalama,” alisema Bw Gakunga.

Ukaguzi

Alitoa mwito kwa wenye magari za usafiri wafanye hima kupeleka magari hayo kwa ukaguzi ili kupunguza ajali.

“Wamiliki wa magari waache tamaa ya kutajirisha haraka kwa kuachia madereva nafasi ya kuendesha magari kwa kasi,” alisema Bw Gakunga.

Afisa mkuu wa kukagua vidhibiti mwendo kwa njia ya kiteknolojia wa E-Kas Technology Bw Wambugu Nyamu, alisema umefika wakati serikali inafaa kuchukua hatua kali kwa wahusika wa ajali zinazoshuhudiwa kila mara.

Alisema mwaka 2018, wasafiri wapatao 3,200 waliangamia kufuatia ajali mbaya za barabarani. Halafu kwa muda wa miaka kumi ambayo imepita “tumepoteza wasafiri wapatao 31,500¬† kwenye ajali.”

Naye afisa mkuu wa polisi eneo la Matuu, Bw John Karanja, alitaja ajali hiyo ya juzi kama ya kusikitisha kwani watu wapatao 14 walifariki papo hapo huku 27 wakijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali tofauti jijini Nairobi.

“Ninatoa mwito kwa wamiliki wa magari ya usafiri wafuate sheria zilizowekwa kwa kutundika vidhibiti mwendo katika magari yao na kuajiri madereva wenye maadili ambao wanastahili kufuata sheria zote za trafiki,” alisema Bw Karanja.

Mwenyekiti wa chama cha kudhibiti usalama barabarani, Road Safety Kenya Association, Bw David Njoroge Kiarie (katikati) pamoja na maafisa wenzake wakikagua eneo la ajali katika mji wa Matuu, mnamo Ijumaa, Machi 29, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

 

 

Basi la Medina Bus kutoka Wajir, lililopata ajali mjini Matuu. Picha/ Lawrence Ongaro