Habari Mseto

Wamiliki wa matatu wasubiri mwongozo mpya

July 8th, 2020 1 min read

Na SAMM WAWERU

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kanuni na mikakati itakayoongoza matatu zitakazoingia na kutoka nje ya kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera itatolewa mnamo Jumatano.

Kauli hiyo imejiri siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuondoa zuio la kuingia au kutoka kaunti hizo, amri iliyowekwa ili kusaidia kuzuia kuenea zaidi kwa Covid – 19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Bw Kagwe Jumanne alisema mwongozo huo utatolewa baada ya kufanyika kwa mkutano na idara ya afya na wadau husika katika sekta ya uchukuzi.

Alisema, kati ya ajenda zitakazojadiliwa ni masharti yatakayotekelezwa kwenye matatu.

“Tukijiandaa kutoa mwongozo huo wenye masharti na mikakati zaidi kesho (Jumatano), wahudumu wa matatu wahakikishe umbali kati ya mtu na mwenzake unazingatiwa, abiria wanawe mikono na lazima wawe wamevalia barakoa (maski) kabla ya kuingia kwenye matatu,” Waziri akasema.

Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa Covid – 19, serikali iliagiza matatu zote kupunguza idadi ya abiria wanaobeba mara moja, hadi asilimia 60 ya idadi jumla. Agizo hilo lina maana kuwa, mfano wa matatu ya jumla ya abiria 14, inapaswa kubeba abiria 8 wakati mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth alisema miongoni mwa yanayotathminiwa ni kuhakikisha kila kaunti inaweka mikakati kupima wanaoingia.

“Tunafanya kazi kwa karibu na serikali za kaunti kuhakikisha tumeweka mikakati kupima kiwango cha joto la wanaoingia, kukagua ikiwa wana homa, kikohozi na pia ugumu katika kupumua. Yote yatatekelezwa katika mipaka kuingia kwenye kaunti,” Dkt Amoth akaelezea.

Kufuatia kuondolewa kwa zuio kuingia na kutoka nje ya Nairobi, Mombasa na Mandera, inahofiwa hatua hiyo huenda ikachangia kusafirishwa kwa virusi vya corona kutoka eneo moja hadi lingine.

Aidha, Dkt Amoth alionya ifikapo mwezi Agosti na Septemba 2020, huenda taifa likawa likiandikisha visa mara tatu au hata zaidi kila siku, kuliko vinavyoripotiwa kwa sasa.