Habari Mseto

MATATU: Wamiliki waapa kukaidi sheria ya NTSA wakidai kuhangaishwa

April 29th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WASHIKADAU wa Matatu eneo la Mlima Kenya wamesema watakaidi sheria mpya ya kuweka magari vidhibiti mwendo ilivyoagizwa na Halmashauri ya Usafiri na Usalama barabarani (NTSA).

Sheria hiyo itahusisha magari makubwa kama basi, malori na magari ya kitalii. Mwenyekiti wake Bw Michael Kariuki, alisema sheria hiyo ni ya kuwapunja kwani matatu nyingi zinazoendesha biashara zina madeni mengi na kwa hivyo sheria hiyo itakuwa ni ngumu kufuata.

“Kufuata maagizo hayo ni kazi kubwa ajabu kwa wamiliki wa matatu kwa sababu kidhibiti mwendo moja inauzwa kwa bei ya Sh40,000. Pesa hiyo ni nyingi mno kwa wengine wetu na kwa hivyo ni vyema wabadilishe uamuzi huo,” alisema Bw Kariuki.

Alisema kuna mawakala wengi katika pendekezo hilo na kwa hivyo wangetaka washikadau wote katika sekta hiyo kutoka Mlima Kenya washauriane kwa kina na wahusika ili kupata mwelekeo mwafaka unaostahili.

“Siku hizi watu wengi wamejua vyema ya kwamba sekta ya matatu ina biashara ya kufana na ndiyo sababu watu ambao wanataka kujitajirisha haraka hujiunga na sekta hiyo,” alisema Bw Kariuki.

Alisema vidhibiti mwendo vinavyopendekezwa havina uthibitisho wa uhalali wake na kwa hivyo hawawezi fuata maagizo hayo hadi kuwe na maelewano ya kuridhisha kutoka kwa wahusika wote.

Alisema mwaka wa 2014 walilazimisha wenye Matatu kutundika vithibiti mwendo zisizo na kasoro, lakini baada ya miezi miwili pekee zilileta shida na kuharibika.

” Hata Halmashauri ya usafiri na usalama wa barabara na kitengo cha trafiki kinaelewa maswala hayo vyema,” alisema Bw Kariuki.

Zaidi ya washika dau 100 walikongamana mjini Thika kujadiliana kuhusu sheria hiyo ambao waliapa hawatafuata hadi sheria ifuatwe ipasavyo.

” Tunajua wengi wetu wana madeni makubwa na hata wengine magari yao yako kwenye vituo vya Polisi kwa makosa tofauti. Hayo yote ni shida yanayostahili kutatuliwa kwanza ili kupiga hatua nyingine,” alifafanua Bw Kariuki.

Alisema iwapo matatu 400 hivi zitalazimishwa kufuata maagizo hayo bila shaka watapata hasara ya takribani Sh 30 milioni.

Alizidi kufafanua kuwa eneo la mlima Kenya lina endesha matatu zaidi ya 5,000 na wanahofia wakifuata maagizo hayo wengine wanahofia kupoteza takriban Sh30 bilioni.

Mshika dau wa Matatu kutoka Thika Bw John Kiarie alisema kwa chini ya miaka michache tu wamelazimishwa kutundika vithibiti mwendo Mara Tatu.

” Wakati huu watu wana mashida mengi kifedha hata wengine wanajipanga kuchukua mikopo ili kuwapeleka wana wao shuleni. Sisi Tunataka tupewe muda ili tujipange vyema,” alisema