Habari Mseto

Wamkata kichwa wakidai aliiba miwa

June 9th, 2020 1 min read

Na GERALD BWISA

Mwanamume wa miaka 75 amekumbana na mauti alipokatwa kichwa na washambuliaji wanaojulikana baada ya kusemekana kuiba miwa kutoka kwa shamba moja kijiji cha Buyanji, Kaunti ya Trans Nzoia.

Bw Gabriel Wekesa ambaye ni mzee wa kijiji aliiambia Taifa Leo kwamba mwanamume huyo kwa jina Edward Khalakai Wanjala alikatwa kichwa kwa panga baada ya kufumaniwa akiiba miwa.

“Nilipokea habari kwamba kuna mtu amepatikana akiiba miwa na akauliwa na vijana wawili,” alisema.

Wakazi wenye hamaki walisema kwamba mtu huyo hakuwa na hatia na kuvamia nyumba ya washambuliaji hao. Washukiwa walitoroka baada ya kufanya kitendo hicho.

“Mzee huyo aliyeishi kijijini kwa miaka 30 amekuwa akitegemea kukata nyasi ili kukujitafutia chakula, wameua mtu asiye na hatia na wakatupa mwili wake kwa barabara,” Suzan Nanjala alilia.

Polisi waliotembealea eneo la matukio walikuta mwili wa Bw Wanjala ukiwa kando ya barabara huku miwa ikiwa kando yake.

OCPD wa eneo hilo Alphonse Kimanzi aliambia Taifa Leo kwamba mwili huo ulikuwa umekatwa kichwa, mguu wa kulia na alama ya pigo mgogoni. Alisema mwili huo ulipelekwa kwenye kituo cha kuhifadhi mahiti cha Hospitali ya kitale.