Habari Mseto

Wamlilia Kibicho kuhusu genge Maragua

August 14th, 2020 2 min read

Na MWANDISHI WETU

WENYEJI wa Murang’a Kusini wamemtaka Katibu wa Usalama wa Ndani Karanja Kibicho atume kikosi maalum cha kupambana na genge hatari la mauaji ambalo linadaiwa kuua watu watano na kujeruhi wengine 20 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Walisema kuwa kituo cha polisi cha Maragua hakiwezi kuaminiwa wajibu huo na kwamba baadhi ya maafisa hupokezwa hongo ili kuwalinda wahalifu hao.

Mshirikishi wa Mpango wa Usalama wa Nyumba Kumi eneo hilo Joseph Mutua alisema kuwa maeneo ambayo ni ngome ya genge hilo ni vijiji vya Maica Ma Thi, Gikindu na Gititu na ambapo katika mji wa Maragua, genge hilo huwa na washirika wa kike ambao husaidia na kuwapa maficho na kuwawekea silaha na mihadarati na pombe aina ya chang’aa na pia kuwatekelezea ujasusi wa uvamizi na kisasi.

Alisema wanawake hao huishi katika mitaa ya Mathare, Soweto, Boarder na Rurii.

Bw Mutua alidai kuwa manaibu wa machifu wa Kianjiru-ini na Gakoigo wametepetea kazi kiasi kwamba genge hilo hupika chang’aa ambayo huuzwa kwa njia ya uwazi huku vituo vya doria vya polisi vya Gakoigo na Mugumo-ini vilivyo chini ya amri ya Kamanda wa Polisi wa Maragua Francisca Mbinda avikilemeewa na kuthibiti hali.

Aidha, Bw Mutua alisema kuwa gari la polisi la Maragua halitolewi kuwajibikia genge hilo na biashara hizo haramu “ili kulinda maslahi ya pato haramu ambalo genge hili hutoa kwa maafisa.”

Bw Mutua alisema kuwa wamepasha Bw Kibicho, Kamishna wa Kaunti Bw Mohammed Barre na Katibu wa baraza la mawaziri Bw Kennedy Kihara kuhusu hali hii, wote ambao walithibitishia Taifa Jumamosi kuwa wamepokea malalamishi hayo.

Juhudi zetu za kumfikia Bi Mbinda kutoa msimamo wake kuhusu madai hayo yaligonga mwamba kwa kuwa hakupokea simu au kujibu ujumbe wetu.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi wa eneo hilo Bw Anthony Keter alisema kuwa amepokezwa madai hayo na uchunguzi wa kina unatekelezwa.

“Ndio, nimepata ujumbe kwamba kuna wakati gari la polisi wa Maragua lilihitajika na wadau wa kiusalama eneo hilo kushughulikia wafuasi wa genge hili waliokuwa wakihangaisha raia lakini likawa eti limeenda Kaunti ya Machakos kuhamisha mtoto wa afisa mmoja wetu. Ni madai ambayo yana uzito na yanachunguzwa. Lakini suala la genge hilo tayari tunalishughulikia kwa kina na tayari tumeanza kulivunja,” akasema.