Habari Mseto

Wamuua kaka yao wakipigania mahari ya dada

October 29th, 2020 1 min read

Na Titus Ominde

FURAHA ya kupokea pesa za mahari katika familia moja katika kijiji cha Cheplachabei, Kaunti Ndogo ya Soy iliyo Kaunti ya Uasin Gishu, iligeuka kuwa karaha baada ya ndugu wawili kumuua kaka yao wakizozania mahari ya dada yao.

Polisi walifanikiwa kukamata wawili hao na kuwazuilia katika kituo cha polisi cha Soy.

Wawili hao Jacob Kipkosgei, 27, na Daniel Kipchirchir, 44, wanadaiwa kumuua Darius Kiplimo. Inadaiwa mzozo uliibuka kuhusu jinsi wangegawana pesa ambazo kiasi chake hakijulikani ambazo baba yao alikuwa amepokea kama mahari kutoka kwa bintiye aliyeolewa hivi majuzi. Marehemu alivamiwa akakatwakatwa kwa panga na kisu.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi katika Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Ayub Gitonga alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

“Ni huzuni kwa mzee huyu kupoteza mtoto wake kutokana na mzozo wa mahari. Kwa sasa familia hii imepata pigo mara mbili ikiizangatiwa kuwa wawili hao wako katika na seli mwingine amefariki,” alisema Bw Gitonga.