Habari Mseto

Wanabodaboda Kiambu waahidiwa mikopo ya riba nafuu

November 13th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu imeweka mikakati ya kuwainua wanabodaboda kibiashara kutokana na matukio ya hali ngumu ya kiuchumi kutokana na makali ya virusi vya corona.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro amesema kuna haja ya kuwajali wafanyibiashara wa chini ili waweze kujikwamua kutokana na hali ngumu ya maisha.

Aliyasema hayo Ijumaa eneo la Githurai, Ruiru  alipowahutubia wanabodaboda huku akiwaonya wajichunge kutokana na corona ambayo imeingia kwa awamu ya pili.

Alisema wanaelewa vyema biashara nyingi zilikwama wakati wa homa ya corona na kwa hivyo ni vyema kuingilia kati kuona biashara za chini zinainuka tena.

Alifichua kuwa tayari wamezungumza na benki kadha ili ziweze kutoa mikopo ya riba ya nchini kwa wafanyabiashara.

“Tutakubaliana nao ili waweze kutoka riba ya asilimia 7 badala ya asilimia 13. Tunataka kuona biashara zikiinuka tena kama hapo awali,” alisema gavana huyo.

Alisema kuna mipango inayoendelea kuona ya kwamba wanabodaboda wanapitia mafunzo kadha ili kuhamasishwa jinsi ya kuzuia ajali nyingi zinazoshuhudiwa kila mara.