Habari Mseto

Wanabodaboda kufunzwa mbinu za kuzalisha wajawazito

July 23rd, 2018 1 min read

Na NDUNG’U GACHANE

WAHUDUMU wa bodaboda katika Kaunti ya Murang’a hivi karibuni watafunzwa jinsi ya kusaidia kuzalisha wanawake wajawazito na kutoa huduma ya kwanza ya matibabu kwa waathiriwa wanaojeruhiwa katika ajali baada ya bunge la kaunti kupitisha mswada wa kutaka afisi ya gavana ibuni sera aina hiyo itakayopelekea kuwepo kwa ambulensi za bodaboda.

Kulingana na madiwani, sera hiyo itapelekea wahudumu 200 wa bodaboda katika wadi zote 35 kufundishwa ili kupunguza maafa ya watoto wanapozaliwa na watu wanaojeruhiwa katika ajali.

Kulingana na diwani maalumu Habire Chege, ambaye alidhamini mswada huo, alichukua hatua hiyo baada ya mtoto katika wadi wa Kariara, Kaunti Ndogo ya Gatanga, kufariki alipofikishwa hospitalini baada ya kuvuja damu kutoka kwa jeraha alilopata alipobebwa kwa bodaboda.

“Inahitajika tuwape uwezo wahudumu wetu wa bodaboda ili kusaidia kuwapa matibabu watu wanaojeruhiwa ajalini, kina mama wajawazito ambao huishia kujifungua barabarani na kuhatarisha maisha ya watoto wao.

“Waziri wa afya katika kaunti anahitajika kubuni mwongozo wa kuwapa wahudumu hao mafunzo ya kimsingi, atambue maeneo ya kaunti ambayo yatanunuliwa ambulensi za bodaboda ili mpango huu uanzishwe kabla mwaka ukamilike,” akasema Bw Habire alipowasilisha mswada huo bungeni.

Huku akiunga mkono mswada huo, Diwani wa Kariara, Bw Joell Murigi, alisema ambulensi ya bodaboda itaimarisha shughuli za ambulensi kumi zilizopo katika kaunti kwani zitakuwa zikifika hadi maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa kwa magari.

Mswada huo uliungwa mkono na madiwani wote 50.