Michezo

Wanabunduki Arsenal wakaa ngumu na kuondoka na pointi tatu licha ya majaribu mengi

April 28th, 2024 1 min read

NA TOTO AREGE

ARSENAL walihakikisha wamezoa alama zote tatu kutoka kwa mahasimu wao wa jadi Tottenham Hotspur Jumapili, kutokana na ushindi wa 3-2 katika Debi ya London iliyochezwa ugani Tottenham Hotspur.

Matumaini ya The Gunners ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) sasa yako hai wakiwa kileleni mwa jedwali na alama 80 baada ya mechi 35.

Ilikuwa tofauti kabisa wakati Arsenal walipochukua uongozi dakika 15 wakati Pierre-Emile Hojbjerg alipounganisha kona ya Bukayo Saka kabla ya Saka kufunga bao la pili dakika ya 27.

Mjerumani Kai Havertz alifunga bao la ushindi kupitia kichwa kutokana na kona ya Declan Rice dakika ya 38.

Ingawa Spurs ilijaribu kurejea mchezoni baada ya kupata mabao kutoka kwa Cristian Romero kufuatia masihara ya kipa David Raya dakika ya 64 na penalti kutoka kwa Son Heung-min dakika ya 87, Arsenal ya kocha Mikel Arteta ilikaa ngumu na kuvuna ushindi muhimu.

Mechi hiyo ilionekana kuwa moja ya mechi kali zaidi zilizowahi kushuhudiwa msimu huu katika ligi ya EPL. Arsenal waliitumia vyema udhaifu wa ulinzi wa Spurs kuanzisha uongozi wa mabao matatu kabla ya mapumziko.