Michezo

Wanachama 6 wa bodi ya Barcelona wajiuzulu

April 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANACHAMA sita wa Bodi ya Usimamizi ya Barcelona wamejiuzulu na kumweleza Rais Josep Bartomeu Maria kwamba hawajafurahishwa na namna ambavyo kikosi hicho cha Ligi Kuu ya soka nchini Uhispania kinavyoendeshwa.

Katika barua iliyoandikwa na kutiwa saini na sita hao, masuala kuhusu jinsi Barcelona itakavyoathirika kifedha kutokana na mlipuko wa sasa wa virusi vya corona pia yalifichuliwa.

Aidha, wanachama hao walikashifu namna ambavyo sakata ya Februari 2020 iliyohusisha Barcelona na hatua ya kushirikiana na kampuni moja nchini Uhispania kuvamia wachezaji wake kupitia mitandao ya kijamii ilivyoshughulikiwa.

Isitoshe, vinara hao walitaka Kamati Kuu ya Barcelona kufutilia mbali Bodi nzima iliyopo kwa sasa na kuagiza uchaguzi mpya wa urais.

Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliojizulu hapo jana ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.

“Tumeifikia hatua hii kwa sababu hatuwezi kubadilisha jinsi Barcelona inavyoendeshwa kwa sasa wakati ambapo kikosi kinakabiliwa na changamoto za kila sampuli, ikiwemo homa ya corona,” ikasema sehemu ya barua hiyo.

“Pia tulifadhaishwa sana na tukio la kusikitisha ambapo Barcelona ilishirikiana na kampuni ya Barcagate kuwazomea na kuwabagua wachezaji kwa misingi ya rangi yao kupitia mitandao ya kijamii,” ikaendelea.

“Mwisho, tunapendekezea usimamizi kuamrisha kuandaliwa kwa uchaguzi mpya wa wadhifa wa urais ili kurejeshea Barcelona hadhi yake ya zamani na kuhakikisha kwamba kikosi kinajivunia uongozi bora utakaokiwezesha kukabiliana na changamoto za hivi sasa na za baadaye,” ikasema barua hiyo.

Katika majibu yao, Barcelona walisisitiza kwamba wamefanikiwa pakubwa katika soka ya Uhispania na bara Ulaya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uongozi murua wa Bartomeu na baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na wanachama sita waliojiuzulu yatajadiliwa kwa kina katika kipindi cha siku chache zijazo.

Katika taarifa yao, pia walifichua kwamba wamekuwa wakiandaa mkutano wa kujadili mbinu mwafaka zaidi zitakazoimarisha kikosi hicho ambacho kimekuwa miongoni mwa klabu bora zaidi duniani kwa miaka mingi.

“Mikakati ya kudumisha ubora wa kikosi pamoja na athari za hivi sasa na za baadaye za corona kwa ustawi wa klabu ni kati ya mambo ambayo yanatarajiwa kuzamiwa kwa kina katika kikao hicho kitakachofanyika hivi karibuni,” ikatanguliza taarifa hiyo.

Kutokana na mlipuko wa corona ambayo imefanya Uhispania kuwa nchi ya pili baada ya Italia iliyoathirika zaidi barani Ulaya, wachezaji wa Barcelona wameafikiana kukatwa mshahara kwa hadi asilimia 70 ili kuwawezesha kuwadumisha baadhi ya vibarua wao kifedha na kutoa msaada wa chakula na vifaa vya afya kwa maelfu ya familia zilizoathirika hasa katika eneo la Catalonia.