Habari Mseto

Wanachama wa Urithi Housing Co-operative wahimizwa kulipa madeni

May 15th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha Ushirika cha Urithi Housing Co-operative Society Ltd, kimeanza kampeni kali ya kukamilisha miradi yake ya maendeleo iliyokwama hapo awali.

Mwenyekiti wake Bw Samuel Maina, alisema madeni wanayodai kutoka kwa wanachama ni Sh2 bilioni; jambo ambalo limelemaza juhudi za chama kupiga hatua zaidi.

Akizungumza na wanachama wake katika shamba la Panorama Gardens eneo la Gatanga Kaunti ya Murang’a, mnamo Jumanne, alisema wanaelewa vyema hali ngumu ya kiuchumi inayowakumba wananchi lakini aliwahimiza wajikakamue ili kulipia madeni yao.

Alisema wanachama kutolipa madeni yao kwa muda ufaao husababisha miradi mingi kusimama.

“Tunawahimiza wanachama wetu wafanye kweli ili kulipa madeni yao  wakati uliowekwa  ili nayo afisi yake iweze kukamilisha miradi  ya ujenzi wa nyumba jinsi walivyopanga,” alisema Bw Maina.

Wakati wa hafla hiyo Bw Maina aliandamana na naibu wake Bw John Gachoka, mwekahazina Kevin Muthuri, na mkurugenzi Bw Julius Gachanja.

Wanachama zaidi ya 800 walihudhuria hafla hiyo huku kila mmoja akipewa nafasi ya kujieleza na kuuliza maswali katika mkutano uliokuwa na msisimko wa kila aina.

“Tunawaomba mtusaidie kwa kulipa madeni yenu haraka iwezekanavyo ili nasi tuwafanyie kazi  kwa njia ya unyenyekevu,” alisema Bw Maina.

Alisema wanataka kuona ya kwamba kwa muda wa miezi sita ijayo wanafanya hima kuona ya kwamba wanakamilisha miradi kadha ya ujenzi wa nyumba walizoanzisha kwa asilimia 80.

Alisema kwa sasa watazunguka kila sehemu wakiwahamasisha wanachama wake umuhimu wa kulipa madeni hayo haraka iwezekanavyo ili kuafikia malengo ya kukamilisha miradi yote.