Habari Mseto

Wanachama wa ushirika waonywa dhidi ya matapeli

May 13th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANACHAMA wa Urithi Housing Co-operative Society Ltd wameshauriwa kuwa macho wasipotoshwe na matapeli.

Mwenyekiti wa chama hicho Bw Samuel Maina, alisema kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na watu fulani wanaozunguka kila mahali wakiwachochea wanachama wao kuwa chama hicho hakina mwongozo ufaao.

“Ningetaka kuwajulisha kuwa hao ni watu walio na kijicho kwa chama hicho kutokana na jinsi kinaendesha mambo yake kwa utaratibu unaostahili. Sisi tunafanya mambo yetu kwa uwazi na sioni ni kwanini wanakuwa na kiwewe na chama chetu,” alisema Bw Maina.

Alisema watu wachache huko nje wamekerwa na jinsi Urithi imepiga hatua kwa kuwatafutia wanachama wake makao kupitia ununuzi wa ardhi huku pia wakipewa  vyeti vya umiliki.

Alizidi kufafanua kuwa Urithi imekuwa katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 7 zilizopita na imeweza kununua ardhi kwa wateja wake katika maeneo tofauti za hapa nchini, huku wakipeana vyeti miliki 6,500.

Alitaja maeneo ambako wamenunua ardhi na kuwauzia wanachama wake ardhi ni Nakuru, Nyeri, Kilifi, Malindi, Nairobi na Thika.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mji wa Thika alipokutana na wanachama wake ili kuwahamasisha umuhimu wa kujinunulia kipande cha ardhi kupitia chama cha Urithi.

“Wale wanaotuharibia jina tuna wachunguza na hivi karibuni tutawataja hadharani kwa sababu wanaonekana kukerwa na jinsi wanachama wengi wa Urithi wamesambaa kila pembe za hapa nchini,” alisema Bw Maina.

Alisema wanazidi kuendeleza ajenda nne za serikali huku wakiwa wamejenga nyumba zipatazo 550.

Alisema kwa wakati huu wanaendelea kukamilisha zingine 1,200 za kiwango ya kadiri kwa gharama ya 500,000 kwa kila moja.