Habari Mseto

Wanachuo kutuzwa mamilioni kwa kuhimiza Wakenya kula wadudu

May 28th, 2018 1 min read

Na ELIZABETH OJINA

WANAFUNZI 80 wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) watanufaika na ufadhili wa Sh600 milioni zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhamasisha Wakenya kula wadudu kama njia mojawapo ya kukabiliana na uhaba wa chakula nchini.

Ufadhili huo unalenga wanafunzi wa uzamili au uzamifu ambao wanafanya utafiti kuhusiana na wadudu wanaolika. Profesa wa Idara ya Chakula chuoni humo, Monica Ayieko alisema kozi na utafiti kuhusiana na ulaji wa wadudu kama chakula mbadala itaanza Septemba, mwaka huu.

“Huu ni mradi wa bara zima, tunaalika wanafunzi kutoka Afrika na kote duniani kwa ajili ya kozi hii,” akasema.

Prof Ayieko alisema tayari mtaala wa kutoa mafunzo ya ulaji wadudu tayari umeandaliwa na unatarajiwa kukaguliwa na kuidhinishwa na Tume ya Kutathmini Elimu ya Juu (CUE) mnamo June 12.

“Tumeandaa mtaala unaojumuisha wadudu wote wanaopatikana kote barani Afrika. Wadudu zaidi ya asilimia 95 wanalika. Tunaweza kutumia wadudu hawa kama chakula mbadala ili kukabiliana na uhaba wa chakula barani Afrika,” akasema.

Alisema afya ya idadi kubwa ya watoto barani Afrika imedhoofika kutokana na ukosefu wa madini muhimu mwilini kama vile vitamini A, Zinki, chuma.

“Wadudu hawa wana madini tele yanayohitajika mwilini. Kwa mfano panzi wana kiwango cha juu cha proteni kuliko nyama na maharagwe. Ni rahisi kukuza na kutunza wadudu,” akasema.