Michezo

Wanaendeleaje mastaa wa Kenya majuu?

September 30th, 2020 5 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Masr anayochezea Mkenya Cliff Nyakeya nchini Misri na HIFK iliyoajiri Arnold Origi nchini Finland ziliona cha mtema kuni uwanjani kwenye Ligi Kuu hapo Septemba 29.

Mambo hayakuwa tofauti kwa Johanna Omolo (Cercle Brugge, Ubelgiji), John Avire (Tanta, Misri), Victor Wanyama (Montreal Impact, Amerika na Canada) na Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan). Hata hivyo, ilikuwa raha tele kwa Eric ‘Marcelo’ Ouma Otieno (AIK Stockholm), Joash Onyango (Simba SC, Tanzania) na Farouk Shikalo (Young Africans, Tanzania) baada ya klabu zao kushinda. Haya hapa matokeo ya klabu za kigeni wanazochezea Wakenya:

Misri

Masr, ambayo mshambuliaji Cliff Nyakeya anachezea, pia inakodolea macho kuangukiwa na shoka. Iko nafasi ya pili kutoka mkiani kwa alama 20 kutokana na mechi 28 katika ligi hiyo ya timu 18. Masr iliaibishwa 6-0 mikononi mwa Arab Contractors hapo Septemba 29 katika mechi ambayo Cliff Nyakeya alisakata dakika zote 90. Raia wa Colombia Luis Edward Hinestroza Cordoba na Mtunisia Seifeddine Jaziri walipachika mabao mawili kila mmoja, huku Wamisri Mohamed Magli na Mohamed Salim wakichangia goli moja kila mmoja. Timu ya Tanta anayochezea mshambuliaji Mkenya John Avire itashiriki Ligi ya Daraja ya Pili msimu ujao baada ya matumaini yake ya kusalia kwenye Ligi Kuu kuzimwa ikichapwa 1-0 Septemba 26 na miamba Al Ahly ambao wameshinda ligi zikisalia michuano minne. Tanta inavuta mkia kwa alama 18 baada ya kushinda michuano yake miwili, kutoka sare mara 12 na kupigwa mechi 16. Tanta na Masr zitarejea uwanjani Oktoba 2 na Oktoba 3 kupepetana na El Gounah na ENPPI, mtawalia.

Belarus

Mohammed Katana Nyanje hakuwa katika kikosi cha Isloch Minskly Rayon kilicholazimisha sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji Energetik-BGU kwenye Ligi Kuu (Vysshaya Liga) hapo Septemba 26. Isloch ilikuwa imeshinda mechi sita mfululizo kabla ya kupigwa breki na Energetik-BGU. Kiungo huyu mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Bandari alisaini kandarasi na Isloch hapo Septemba 22, ingawa amekuwa na timu hiyo kutoka Novemba 2019.

Ubelgiji

Kiungo mkabaji Johanna Omolo, ambaye pia ana uraia wa Ubelgiji baada ya kuishi nchini humo tangu Julai 1 mwaka 2007, hakuwa katika kikosi cha Cercle Brugge timu hiyo yake ikipoteza 2-1 ugenini dhidi ya miamba wa Club Brugge hapo Septemba 27. Cercle inapatikana katika nafasi ya tisa, moja nje ya mwisho ya kuingia Ligi ya Uropa kwenye ligi hiyo ya timu 18. Itarejea uwanjani hapo Oktoba 3 itakapoalikwa na Eupen.

Uingereza

Barnsley, ambayo imeajiri beki Mkenya Clarke Oduor, ilipata alama yake ya kwanza kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uingereza baada ya kutoka 0-0 dhidi ya wageni Coventry hapo Septemba 26. Oduor,21, ambaye amejumuishwa katika kikosi cha Harambee Stars kwa mara ya kwanza, alikuwa kitini mechi nzima. Barnsley, ambayo inashikilia nafasi ya 20, itazuru nambari 18 Middlesbrough katika mechi yake ijayo hapo Oktoba 3.

Finland

HIFK anayochezea kipa Arnold Origi ilikung’utwa 3-2 dhidi ya wenyeji SJK kwenye Ligi Kuu (Veikkausliiga) mnamo Septemba 29. Ilikuwa imetupa uongozi wa mabao mawili ikitoka 2-2 dhidi ya Mariehamn hapo Septemba 19 kabla ya kudondosha alama zote dhidi ya SJK. HIFK iko alama mbili juu ya kundi la mduara wa kutemwa katika nafasi ya sita kwenye ligi hiyo ya klabu 12. Origi amekuwa michumani mechi sita zilizopita. HIFK itakaribisha nambari nne Honka katika mechi ijayo hapo Oktoba 2.

Ireland

Cork City inasalia mkiani mwa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Ireland katika nafasi ya 10 baada ya kuambulia alama moja katika sare ya 1-1 dhidi ya nambari tisa Finn Harps hapo Septemba 27. Timu ya Cork haikuwa na kiungo Henry Ochieng’ kikosini. Ochieng’ alikuwa akitumikia marufuku ya mechi moja. Cork, ambayo itakuwa mwenyeji wa nambari sita St Patricks hapo Oktoba 3, imezoa alama tisa kutokana na mechi 12.

Japan

Mshambuliaji Michael Olunga alifunga bao lake la 17 kwenye Ligi Kuu ya J1 League msimu huu, lakini halikutosha kuepushia Kashiwa Reysol kichapo cha magoli 3-1 dhidi ya mabingwa watetezi Yokohama F. Marinos hapo Septemba 27. Olunga aliweka Reysol kifua mbele dakika ya 40 kabla ya Marinos kujibu na mabao matatu kutoka kwa Erik Lima, Takuma Ominami (bao la kujifunga) na Daizen Maeda katika dakika 13 za mwisho. Kashiwa inapatikana katika nafasi ya nane kwa alama 30 bega kwa bega na nambari tisa Urawa Red Diamonds kwenye ligi hiyo ya timu 18. Olunga yuko mabao sita mbele ya Everaldo (Kashima Antlers), Marcos Junior (Yokohama F. Marinos) na Yu Kobayashi (Kawasaki Frontale). Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kuwa uwanjani kusaidia timu yake ya Kashiwa kutafuta alama itakapokutana na Yokohama FC hapo Oktoba 3.

Uswidi

AIK Stockholm anayochezea Mkenya Eric “Marcelo” Ouma Otieno iko nje ya mduara hatari wa kutemwa kwa alama tatu katika nafasi ya 12 baada ya kuzima nambari tisa Mjallby 1-0 hapo Septemba 28. Marcelo amekuwa nje tangu Mei mwisho alipoumia mguu mazoezini na kufanyiwa upasuaji. Anakaribia kurejea ulingoni.

Beki Joseph Stanley Okumu alirejea katika kikosi cha Elfsborg baada ya kukosa mechi iliyopita akiugua mafua katika sare tasa dhidi ya Goteborg hapo Septemba 27. Elfsborg haijashinda mechi saba mfululizo. Inashikilia nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Allsvenskan kwa alama 36, nyuma ya nambari mbili Norrkoping kwa tofauti ya ubora wa magoli. Malmo iko kileleni kwa alama 44 kwenye ligi hii ya timu 16. Mechi ijayo ya AIK itakuwa dhidi ya nambari nane Ostersunds hapo Oktoba 4.

Naye mshambuliaji Eric Johana Omondi aliingia uwanjani dakika ya 80 timu yake ya Jonkoping Sodra ikatoka 2-2 dhidi ya Vasteras mnamo Septemba 27. Aliingia uwanjani dakika chache tu baada ya Vasteras kurejesha goli moja kupitia Emil Skogh. David Engstrom aliongeza bao la pili la Vasteras sekunde chache kabla ya mechi hiyo kutamatika na kunyima ushindi Jonkopings, ambayo ilikuwa imeona lango kupitia Amir Al Ammari (penalti) na Moustafa Zeidan katika dakika ya 42 na 63, mtawalia. Jonkopings inashikilia nafasi ya tatu, ambayo ni ya mwisho ya kuingia Ligi Kuu. Jonkopings inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili, itagaragazana na nambari mbili Halmstad hapo Oktoba 3.

Nayo Vasalunds wanayochezea Anthony Wambani na Michael Ovella Ochieng’ iliendelea kujiweka pazuri kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Daraja ya Pili baada ya kuchabanga Orebro Syr. 2-1 hapo Septemba 26. Vasalunds imefungua mwanya wa alama nane baada ya kuzoa alama 50 kutokana na mechi 20 kwenye ligi hiyo ya timu 16. Ushindi huo ulikuwa wa Vasalunds wa tano mfululizo. Wambani alishiriki mechi hiyo nzima, lakini Ovella hakuwepo kwa mara yake ya 11. Vasalunds itakabana koo na Haninge katika mechi yake ijayo mnamo Oktoba 4.

Tanzania

Simba SC, ambayo imeajiri beki Joash Onyango na kiungo Francis Kahata, ilizaba Gwambina 3-0 Septemba 26 jijini Dar es Salaam nayo Young Africans (Yanga) anayochezea kipa Farouk Shikalo ikalima Mtibwa Sugar 1-0 Septemba 27. Shikalo alikuwa kwenye benchi ya Yanga naye Onyango alichezea Simba, huku Kahata akikosekana kabisa. Azam inaongoza kwa alama 12 baada ya kushinda michuano yake minne ya kwanza ikifuatiwa na mabingwa watetezi Simba (10) na Yanga (10) mtawalia. Mechi ijayo ya Yanga na Simba itakuwa dhidi ya nambari 14 Coastal Union na nambari 13 JKT Tanzania mnamo Oktoba 3 na Oktoba 4, mtawalia. Biashara Mara United, ambayo inanolewa na Mkenya Francis Baraza, inashikilia nafasi ya saba kwenye ligi hiyo ya timu 18 baada ya kutoka 0-0 dhidi ya Ruvu Shooting hapo Septemba 27. Vijana wa Baraza watajibwaga uwanjani dhidi ya nambari tisa Mtibwa Sugar katika mechi ijayo mnamo Oktoba 4.

Amerika na Canada

Montreal Impact ya kocha Thierry Henry ilipoteza mechi yake ya nne mfululizo ilipopigwa 4-1 na New York Red Bulls kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) mnamo Septemba 28. Nahodha wa Kenya, Victor Wanyama alichangia pasi iliyofungwa na Mhispania Bojan Krkic kwenye ligi hiyo katika ukanda wa Mashariki. Montreal inashikilia nafasi ya nane kwa alama 16 baada ya kusakata mechi 14 kwenye ligi hiyo ya Mashariki ya timu 14 inayoongozwa na Columbus Crew. Seattle Sounders, ambayo imeajiri Mkenya Handawalla Bwana, inaongoza ukanda wa Magharibi kwa alama 24 kutokana na mechi 13 baada ya kulaza Los Angeles Galaxy 3-1 mnamo Septemba 28. Mshambuliaji Bwana hakujumuishwa kikosini. Montreal Impact itaalika nambari 10 Chicago Fire nayo Seattle Sounders ikabiliane na nambari 10 Vancouver Whitecaps katika mechi zijazo Oktoba 4.