Wanafunzi 2,000 Mukuru wapigwa jeki kielimu

Wanafunzi 2,000 Mukuru wapigwa jeki kielimu

Na SAMMY KIMATU

WANAFUNZI zaidi ya 2,000 wamepigwa jeki kielimu baada ya kampuni moja kuahidi kutoa msaada kwa watoto hao eneo la Mukuru.

Maafisa kutoka kampuni ya Lions Head walitembelea shule mbili za msingi zinazosimamiwa na Mukuru Promotion Centre (MPC) katika eneobunge la Makadara, kaunti ya Nairobi.

Aidha, walizuru katika shule ya msingi ya Sancta Maria-Mukuru na shule ya msingi ya St Catherine ili waone ni msaada upi watakaotoa.

Shule hizo ni za umma.

Zaidi ya hayo, mkurugenzi mkuu wa MPC, Mtawa Mary Killeen aliambia wanahabari kwamba kampuni hiyo itashirikiana na wafadhili wengine-Team Pankaj kufadhili shule zoteb mbili.

“Kampuni ya Lions Head itashirikiana kutoa msaada wake na wenzao wa Team Pankaj-kundi la wahisani wa hapa nchini ambao hutoa msaada wa chakula kwa wanafunzi zaidi ya 6,000 katika shule zetu za MPC,” Mtawa Mary akasema.

Hata hivyo, mtawa Mary aliongeza kwamba kampuni hiyo haikufafanua zaidi ni msaada wa aina gani watatoa ila kusema watapanga na kuamua kisha kutangaza watasaidia shule hizo kwa namna gani.

MPC ni shirika la kidini linalotoa msaada kwa wanafunzi katika shule nne za msingi, moja ya upili, kituo cha watoto wanaorandaranda mitaani na kituo cha mafunzo ya kiufundi.

Wanafunzi katika shule zote huwa ni watoto kutoka familia maskini katika maeneo ya Mukuru.

Mtawa Mary alisema shule hizo ni pamoja na shule ya msingi ya St Elizabeth, Shule ya msingi ya St Bakhita na Shule ya msingi ya Mukuru.

Shule nyingine ni Shule ya Msingi ya St Catherine, Shule ya Upili ya St Michael, Mary Immaculate Rehab na Mukuru Vocational Skills Training Centre.

Vilevile, Shule ya Msingi ya St Elizabeth iko katika tarafa ya Viwandani kwenye kaunti ndogo ya Makadara.

Shule ya St Bakhita, Mukuru, St Catherine, Shule ya Upili ya St Michael, Mary Immaculate Rehab na Mukuru Vocational Skills Training Centre zimo ndani ya tarafa ya South B, kwenye kaunti ndogo ya Starehe.

Baadhi ya wanafunzi katika shule hizi ni pamoja na mayatima, watoto ambao akina mama hawajaolewa, watoto waliookolewa na polisi na wengine kutoka makao ya watoto mbalimbali.

“Tuko na mseto wa watoto wa aina mbalimbali na walio na historia za huzuni ambao bila shaka ukisimuliwa maisha yao utawahurumia na kuona ni kweli wanastahili kusaidiwa na kupewa fursa ya kujiendeleza kielimu,” Mtawa Kileen akaeleza.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa biriani ya nyama ya ng’ombe

Kipusa Viviane Miedema atawazwa Mwanasoka Bora wa Kike...

T L