Wanafunzi 3 wa chuo kikuu waliotekwa nyara wauawa

Wanafunzi 3 wa chuo kikuu waliotekwa nyara wauawa

Na AFP

LAGOS, Nigeria

WANAFUNZI watatu waliotekwa nyara wameuawa kwa kupigwa risasi na wahalifu, afisa mmoja wa serikali ya Nigeria alisema Ijumaa.

Afisa huyo alieleza hayo siku tatu baada ya wanafunzi hao kutekwa na watu wenye bunduki chuoni mwao kaskazini mwa nchi hiyo.

Mauaji ya wanafunzi hao yanajiri wakati ambapo visa vya utekaji nyara vimekithiri maeneo ya kaskazini na kati mwa Nigeria ambapo magenge ya wahalifu hushambulia vijiji na kusababisha uharibifu wa mali.

Wahalifu wenye bunduki walishambulia Chuo Kikuu cha Greenfield katika jimbo la Kaduna mnamo Jumanne, wakaua mfanyakazi mmoja na kuteka nyara idadi isiyojulikana ya wanafunzi.

Hicho ni kisa cha tano ambapo shule au vyuo hushambuliwa na wanafunzi kutekwa nyara nchini Nigeria tangu Desemba mwaka jana.

“Wahalifu wenye bunduki ambao waliwateka nyara wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Greenfield wamewaua kwa kuwapiga risasi watatu kati ya mateka wao,” akasema Samuel Aruwan, ambaye ni kamishna wa usalama wa ndani katika jimbo la Kaduna, akiongeza kuwa idadi isiyojulikana ya wanafunzi walitekwa na wahalifu hao.

Maiti za wanafunzi hao zilipatikana katika kijiji kimoja karibu na chuo hicho, akasema kwenye taarifa.

Wafanyakazi wawili wa chuo hicho kikuu cha Greeenfield waliambia shirika la habari la AFP kwamba wanafunzi 20 na wahadhiri watatu walitekwa nyara, lakini maafisa wa jimbo hilo hawakuthibitisha takwimu hizo.

Katika miezi ya hivi karibuni majambazi wamekuwa wakiwateka nyara wanafunzi kwa lengo la kulipwa ridhaa na serikali na wazazi wa wanafunzi hao.

Lakini serikali ya jimbo la Kaduna imeshikilia kuwa haitatoa malipo kama hayo kwa wahalifu.

“Hatutawapa pesa zozote na hawatachuma faida yoyote kutoka jimbo la Kaduna,” gavana Nasir Ahmad El-Rufai aliwaambia wanahabari mapema mwezi huu.

Habari za kuuawa kwa wanafunzi hao zilijiri saa kadhaa baada ya Rais Muhammadu Buhari kulaani vifo vya “makumi” ya wanakijiji wiki hii mapema wiki hii katika jimbo jirani la Zamfara. Kiongozi huyo aliwaamuru maafisa wa usalama kuwawinda wahuni hao.

Rais alisema huenda karibu watu 60 waliuawa katika uvamizi katika vijiji kadha katika jimbo hilo lakini ni miili tisa pekee iliyopatikana.

Polisi na maafisa wa serikali hawangethibitisha idadi kamili ya waliouawa.

Kwenye taarifa Alhamisi jioni Rais Buhari alisema “mauaji hayo ya kinyama yatakomeshwa hivi karibuni,”

Aliviamuru vikosi vya usalama kupambana na wahalifu hao kwa lengo la kurejesha usalama katika jimbo hilo.

Wakazi walisema wavamizi wenye silaha waliokuwa wakisafiri kwa pikipiki walivamia vijiji 13 katika mji wa Magami jimboni Zamfara Jumatano jioni. Waliwafyatulia risasi wananchi na kuteketeza nyumba.

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Sasa ni wakati bora wa kuzidisha...

JAMVI: Utata wa BBI tishio kwa Handisheki