Habari Mseto

Wanafunzi 3 waliokutwa wakichungulia ndani ya kantini waruhusiwa kurudi shuleni

March 12th, 2020 2 min read

Na BRENDA AWUOR

WANAFUNZI watatu kutoka shule ya upili ya wavulana Chulaimbo, Kisumu, wameruhusiwa kurudi shuleni baada ya kufukuzwa kwa kukutwa Jumatatu wakichungulia chapati katika kantini.

Wazazi wawili wa wanafunzi waliofukuzwa shuleni ikidaiwa walipatikana na hatia ya kuchungulia chapati katika kantini Jumatatu, saa tatu usiku wakati wanafunzi wenzao wakiwa madarasani kwa masomo ya jioni na usiku, walipokea ujumbe kwamba wana wao wameruhusiwa warudi shuleni.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule siku hiyo ya kufukuzwa kwa wanafunzi mwendo wa saa tatu usiku kuwa nirudishe mwanangu shuleni kutatua suala hiyo,’’ mzazi wa mmoja ameeleza.

Mzazi wa mwanafunzi mwingine akiongea na ‘Taifa Leo’ kwa simu, amesema alipata ujumbe kutoka kwa naibu mkuu wa shule Bw Joshua Ameda, akimwarifu afike shuleni huku ikielezea kuwa mwanawe pamoja na wanafunzi wengine wawili walikuwa wamepatikana wakichungulia chapati katika kantini ya shule.

“Nilipokea ujumbe kutoka kwa naibu mkuu wa shule, kufika shuleni siku ya Jumatano kwa maelezo kuwa mwanangu alipatikana na hatia ya kuchungulia chapati kantini,’’ mzazi alisema.

Aliongeza kuwa naibu mkuu wa shule Bw Ameda, aliwapa wana wao muda wa wiki mbili kukaa nyumbani baada ya kupatikana mbele ya kantini ambapo kwa kipindi cha siku tatu, chapati zilikuwa zimepotea mfululizo.

Inasemekana kuwa chapati 98 zilipotea siku ya kwanza, 60 siku ya pili na 50 kupotea usiku huo mlinzi wa shule alipopata wanafunzi hao wakichungulia chapati.

Wazazi hao walipouliza iwapo wana wao walipatikana na chapati, hawakupata jibu kutoka kwa Bw Ameda ila waliambiwa kuandamana na wana wao nyumbani kwa muda wa wiki mbili kamati ya shule ikipanga mkutano wa kusuluhisha suala hilo.

‘’Tulipouliza iwapo wanafunzi hawa walipatikana na chapati, tulikosa jibu na kuandamana na watoto jinsi tulivyoagizwa,’ ’mzazi wa pili alielezea.

Wazazi hawa waliokataa kujitambulisha walisema kuwa wana wao waliwaelezea kuwa usiku huo walipopatikana na mlinzi wa shule mbele ya kantini, walikuwa wamejikinga mvua baada ya kutoka sehemu ya bweni na hata wakashtushwa walipotuhumiwa kwa wizi wa chapati.

Lakini Mwalimu mkuu wa shule, kupitia mahojiano ya simu, alikana madai kuwa wanafunzi hao walifukuzwa kwa kosa la wizi wa chapati.