Habari Mseto

Wanafunzi 500 hutumia choo kimoja, wengi hukimbilia kichakani

July 17th, 2018 1 min read

Na NDUNGU GICHANE

ZAIDI ya wanafunzi 500 katika Shule ya msingi ya St. Mary iliyoko Kiharu, Kaunti ya Murang’a wamelazimika kutumia choo kimoja baada ya choo cha wavulana kuporomoka wiki iliyopita.

Wanafunzi wote sasa wanatumia choo cha wasichana huku shule ikilazimika kumwajibisha mwalimu mmoja kila siku kudhibiti matumizi ya choo hicho.

Cha kusikitisha ni kwamba wavulana wengi wameamua kutumia kichaka cha karibu kwenda haja baada ya kukataa kutumia choo hicho na wanafunzi wasichana.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Alice Kanyora alitaja hali hiyo kama ya kusikitisha na isipotatutuliwa haraka huenda shule hiyo ikafungwa na mafisa wa afya.

Alisema ameiarifu ofisi ya hazina ya CDF ya eneobunge la Kiharu na serikali ya Kaunti ya Murang’a akilenga kupata jibu litakalosaidia kurekebisha hali hiyo..

“Natumai viongozi waliochaguliwa watatusaidia kwa sababu hali ikisalia hivi huenda tukalazimika kufunga shule,” akasema Bi Kanyora.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha St. Mary, Murathi Magochi ambaye anaishi karibu na shule hiyo, alisema vyoo hivyo vilijengwa 1968 na havijawahi kurekebishwa wala vyoo vipya kujengwa.

“Tunaiomba serikali ya kaunti na hazina ya CDF ya eneobunge la Kiharu waingilie kati na kuokoa wanafunzi hawa ili waweze kuendelea na masomo yao bila matatizo,” akasema Bw Murathi.