Wanafunzi 600 katika wadi ya Nairobi Kusini wapata basari

Wanafunzi 600 katika wadi ya Nairobi Kusini wapata basari

NA SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

MAMIA ya wanafunzi wengi wasiojiweza ambao wanajiandaa kurejea shuleni kwa muhula wa kwanza wa kalenda ya masomo wamepigwa jeki leo Jumatano baada ya diwani kuwagawia hundi za kugharimia kiasi fulani cha karo na ambazo zilikuwa ni za thamani ya Sh3 milioni.

Wazazi na walezi wamemiminika katika afisi za wadi ya Nairobi Kusini zilizoko katika mtaa wa Plainsview South ‘B’, kaunti ndogo ya Starehe, kutafuta fedha hizo.

Walakini, sio kila mzazi alirudi nyumbani akitabasamu kwani mahitaji yalizidi pesa zilizopatikana.

Mwakilishi wadi ya Nairobi Kusini Bi Waithera Chege ameambia Taifa Leo fomu 600 za basari zilikabidhiwa wazazi na walezi wa watoto leo Jumatano.

Mwakilishi wadi ya Nairobi Kusini Bi Waithera Chege akihutubu akiwa katika wadi yake mnamo Januari 25, 2023. PICHA | SAMMY KIMATU

Kila mnufaika atapata Sh5,000 huku Sh3 milioni zikiwa zimetengwa kuwanufaisha wanafunzi katika shule za upili, taasisi na vyuo vingine.

Wazazi wamelalamika kuwa kiasi kilichotengwa kwa ajili ya basari hakitoshi kukidhi mahitaji wala kuwatosha wakazi wa wadi hiyo.

Hata hivyo, Bi Chege amesema wazazi ambao hawajafanikiwa watoto wao kupata basari muhula huu watapewa kipaumbele katika muhula wa pili.

“Wakati huu, serikali inapeana basari mara mbili kwa mwaka – katika Muhula wa Kwanza na wa Pili. Hapo awali, katika serikali za awali, tulitoa basari moja pekee kwa mwaka,” Bi Chege alisema.

Amebainisha kuwa hii itawaondolea wazazi mzigo wa kulipa karo na kusaidia juhudi za serikali kufikia sera yake ya mpito ya asilimia 100.

Bi Chege amekariri kwamba eneo lake limeshuhudia ongezeko la wanafunzi wenye matatizo ya karo, akitaja ukosefu wa ajira ulioletwa na kuachishwa kazi kwa baadhi ya wazazi wakati wa janga la Covid-19.

Ufurushaji wa watu wengi uliotekelezwa mwaka 2022 ili kufungua njia kwa mradi wa nyumba na barabara, ameongeza, pia uliathiria vibaya maisha yao.

Mwakilishi wadi ya Nairobi Kusini Bi Waithera Chege ameambia Taifa Leo wazazi wamekabidhiwa fomu 600 za basari ili kuwafaa wanafunzi wanaokabiliwa na ugumu wa kukamilisha karo. PICHA | SAMMY KIMATU

Vibanda vya kando ya barabara vya maelfu ya wafanyabiashara katika mtaa wa Fuata Nyayo na Mariguini vilibomolewa ili kupisha mradi wa barabara.

“Maelfu ya wakazi walipoteza makazi na biashara zao ili serikali itekeleze mpango wake wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu na mradi wa barabara chini ya Ajenda Nne Kuu za utawala,” amesema.

Aidha anaitaka serikali kushirikiana na wadau katika sekta ya kibinafsi kuhakikisha kwamba wakazi katika mitaa ya mabanda wanaweza kupata nafasi za kazi katika sekta ya viwanda.

  • Tags

You can share this post!

Obiri na Korir kushindania ubingwa wa Ras Al Khaimah Half...

Spika Wetang’ula aharamisha kanuni ya CBK ya...

T L