Wanafunzi 604, 031 kujiunga na mafunzo ya kiufundi

Wanafunzi 604, 031 kujiunga na mafunzo ya kiufundi

Na MARY WAMBUI

VYUO vya mafunzo ya kiufundi vitasajili wanafunzi wote 604,031 waliokosa kupata alama ya kujiunga na vyuo vikuu ya C+.Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha alisema kwamba, wanafunzi wote watasajiliwa katika taasisi hizo.

“Taasisi ya kuteua wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya mafunzo (KUCCPS) imetambua vyuo vikuu 10, vyuo na taasisi za mafunzo anuai ambazo ziko na nafasi za kutosha wanafunzi wote. Taasisi hizi zote zimeelezea uwezo wao kabla ya zoezi la kuchagua watahiniwa wa KCSE mwaka huu,” alisema Magoha.

Alisema shirika hilo linazungumza na mashirika ya kusimamia elimu; Tume ya Elimu ya juu (CUE) na Mamlaka ya Vyuo Anuai (TVETA) ili kuhakikisha taasisi zote zimejiandaa kuwasajili wanafunzi hao kwa mujibu wa azma la serikali la kutoa elimu bora.

Ni wanafunzi 143, 140 waliopata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu nchini ikilinganishwa na 125, 746 mwaka 2019.

“Nawahakikishia wanafunzi ambao watapata matokeo ya leo kwamba, wana kila sababu ya kuwa na matumaini siku za usoni,” alisema Magoha.

Kwa mujibu wa wizara ya elimu, idadi ya vyuo vya kiufundi nchini imeongezeka kutoka 52 mnamo 2013 hadi 233 mwaka huu.Serikali imekuwa ikihimiza wanafunzi wajiunge na taasisi za mafunzo ya kiufundi kuhakikisha kila mmoja anasomea taaluma yake.

You can share this post!

Wavulana wang’aa idadi ya wasichana ikiongezeka

Shule za Pwani zakosa kung’aa KCSE