Wanafunzi kadhaa Juja washindwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa kukosa karo

Wanafunzi kadhaa Juja washindwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa kukosa karo

Na LAWRENCE ONGARO

WAZAZI wengi katika vijiji vya Maraba, Nyachaba na Ndarugu, eneo la Juja, wanataka Wizara ya Elimu kuingilia kati kuwasaidia kwa sababu kuna baadhi ya wanafunzi ambao wameshindwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kutokana na ukosefu wa karo.

Kulingana na baadhi ya wakazi waliohojiwa, wengi wa wanafunzi wamelazimika kufanya shughuli za uchimbaji wa mawe ya ujenzi ili wapate fedha za kujikimu na pia kujitahidi kuwasaidia wazazi wao kupata karo.

Bi Jane Wambui ambaye ni mkazi wa Maraba, eneo la Juja, anasema hadi kufikia sasa mtoto wake wa kiume bado hajaripoti kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa sababu ya kukosa karo.

“Maisha ambayo tunaishi ni magumu kwa sababu mimi na kijana wangu tunafanya vibarua tukipiga mawe eneo la Juja na pesa kidogo tunazopata huingia kwa matumizi ya kununua chakula,” alijitetea mama huyo.

Alisema amejaribu kutafuta fedha za basari lakini amekuwa akielezwa asubiri hadi wakati zitatolewa kwa kila mwanafunzi.

Alisema amejaribu kutafuta wafadhili ili wasaidie lakini hajapata usaidizi wowote.

Alisema wazazi wengi tayari wamesononeka wasijue la kufanya kwa sababu wana wao wengi bado wako nyumbani.

Wakazi hao walisema hata ingawa serikali ilisema wanafunzi wasifukuzwe kutoka shuleni lakini wengi wao wakiripoti wanaelezwa kurejea wakiwa na pesa za karo mkononi.

“Wazazi wengi wanaotoka katika kijiji hiki wanafanya vibarua katika sehemu za kuchimba mawe huku ujira wanaolipwa ukiwa mdogo mno. Sisi tumefika mwisho na tungetaka serikali iseme jambo ili watoto wetu pia waende shuleni kusoma.” akaongeza.

Wanafunzi wengine wameamua kuketi nyumbani wakisononeka huku wakiwa wamepoteza matumaini ya kuendelea na masomo.

Mwanafunzi mmoja aliyehojiwa baada ya kupata idhini ya wazazi, John Mungai kutoka kijiji cha Maraba, alisema yeye alipata alama 331 na bado hajajiunga na Kidato cha Kwanza.

“Tayari naona siku zinayoyoma bila mimi kuripoti shuleni. Kwa hivyo ninazidi kupoteza matumaini. Ninaomba wahisani popote walipo wajitokeza ili wanisaidie niripoti shuleni,” alisema mwanafunzi huyo.

Alisema anahofia ndoto yake ya kuwa mhandisi ni kama itadidimia na kwa hivyo angeomba serikali kuingilia kati haraka iwezekanavyo.

Bw Joseph Kinyanjui wa kijiji cha Nyachaba, eneo la Juja anasema wanafunzi wengi wameachwa kusononeka wasijue la kufanya.

“Sisi kama wazazi tumeshindwa la kufanya kwa sababu jambo hilo likikosa kuangaziwa bila shaka watoto wetu wengi wataingilia mambo maovu huku wakipoteza nafasi yao ya kujiendeleza kimasomo,” alisema Bw Kinyanjui.

Alisema ana watoto wawili ambao walistahili kuanza elimu ya sekondari lakini ni mmoja pekee alipata nafasi hiyo.

“Pesa chache ninazopata huwa ni kidogo za chakula na kwa hivyo sina za karo. Ninaomba wahisani wenye nia njema wajitokeza ili mtoto wangu apate nafasi ya kuripoti shuleni,” alijitetea Bw Kinyanjui.

You can share this post!

Aston Villa wapiga Man-United breki kali ligini

Gavana Ottichilo atimiza ahadi ya kuwapa Vihiga Queens Sh1...