Makala

Wanafunzi KU waunda mapipa ya taka kwa ‘chupa kero’

April 24th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

CHUPA za plastiki zilizotumiwa si lazima zitupwe kwenye jaa la taka sababu huko si makao yao.

Hilo halifanyiki katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) ambapo wanafunzi wanaongeza thamani kwenye taka za plastiki.

Wao hutumia chupa za plastiki kuunda mapipa – badala uzitupe pipani, unazitumia kuunda pipa!

Wanachuo wanafanikisha mpango huu kupitia mpango salama kwa mazingira maarufu Kijani Bin Project.

Wanarika hawa wako mbioni kunadhifisha mazingira yao chuoni na hata nchini kwa kuwa wabunifu na plastiki taka.

Chama cha wanafunzi kinachojinasibisha na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kielimu, Kisayansi na Kitamaduni (KU-UNESCO) huendeleza juhudi za kuhifadhi mazingira.

Wakiendelea kufanyia ubunifu huu majaribio, wanachuo huunda pipa kutumia chupa 60 za plastiki, nyaya na chuma.

Daniel Musembi,19, ambaye ni Meneja Mkurugenzi wa KU-UNESCO, anaamini huu ni mpango mkubwa sana wa kuleta mageuzi ya uhifadhi wa mazingira.

Daniel Musembi aonyesha pipa lililoundwa kwa chupa za plastiki zilizotumika. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Badala ya kutupa chupa za plastiki ovyoovyo, tunakita vituo vya ukusanyaji taka chuoni na viunga vyake ambapo tutakuwa tukikusanya chupa,” alisema.

“Ili kuokoa Dunia, lazima tushirikiane kudhibiti uchafu.”

Chama hiki kinahudumu mwaka wake wanne sasa baada ya kuasisiwa 2020.

“Tulianza shirika hili kwa nia ya kuhamasisha jamii kuhusu Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ushirikiano na ubalozi wa kukabili mabadiliko ya hali ya anga na kutunza mazingira,” alisema Musembi ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Sayansi ya Mazingira.

Msaidizi wake, Adam Furaha, anayesoma Shahada ya Elimu ya Mazingira na Utunzaji Maliasili, pia ni mwanaharakati wa kutetea mazingira.

“Chama hiki kimefanikisha miradi chuoni na viungani kuthibiti uchafu, kukumbatia uvumbuzi na kutoa hamasa ya afya na SDG,” Adam aliambia Taifa Leo.

Adam Furaha aonyesha chupa ya maji iliyorembeshwa kisanaa kwa nyuzi. PICHA | LABAAN SHABAAN

Shirika hili la wanachuo lina wanachama 124 ambao pia huangazia sanaa, utamaduni na stadi dijitali kutekeleza dhima yao.

Wakati mwingine wanabadili mwonekano wa chupa ya kubebea maji ya kunywa wakizirembesha kwa nyuzi.

Taka za plastiki zimekuwa tisho kubwa kwa mazingira sababu ya athari yake kwa afya ya binadamu, usafi na viumbe vya majini.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Mazingira (UNEP), takriban asilimia 20 ya uchafu (bila kuhusisha majimaji na gesi) ni plastiki taka.

Plastiki hizi huchangia zaidi ya asilimia 15 ya uvukaji wa gesi ukaa zinazoongeza viwango vya joto duniani.

“Tukio hili hutupa motisha ya kuzamia udhibiti wa taka za plastiki,” Daniel alikiri.

“Tumevutiwa pia na kuchangamkia suluhu za kibunifu kukabili changamoto za mazingira.”

Mradi wa Kijani Bin Project uko katika hatua za mwanzo na vijana hawa wanaendelea kuboresha majalala kuyakinga dhidi ya mvua kwa kuunda vifuniko.

“Malighafi ya kuunda pipa — chupa za plastiki, nyaya, na gundi — zinapatikana rahisi,” Daniel alisema kwa uchangamfu.

Majaa haya yanatofautiana kwa ukubwa, umbo na malighafi hivyo kuwa na bei mbali mbali.

Lakini, chama kina nia ya kupunguza gharama zaidi.

“Tuna mpango wa kujenga vituo vya ukusanyaji chupa za plastiki. Wateja watakaokuleta chupa hizi wataundiwa mapipa kwa bei ya chini,” Adam alifichua.

KU-UNESCO kinalenga kuuza bidhaa hizi katika taasisi za mafunzo, maeneo ya umma na mashirika mengine.

Mapipa haya yanatumika katika afisi kadhaa KU kama vile Kituo cha Green Education Hub.

“Wakati tunayabeba, mapipa haya huvutia watu sana wakitaka kuyajua na kuyagusa,” Adam alishangaa akiamini ni mvuto wa kibiashara.

Mradi wa Kijani Bin umevutia mashirika yanayowashika mkono vijana hawa mabalozi wa mazingira.

Wazo hili lilikuzwa katika Kituo cha Makuzi na Uvumbuzi wa Biashara cha Chandaria (CBIIC) chini ya Mkurugenzi Prof Maina Mwangi mbaye ni mhadhiri KU.

Baada ya kuwa wakala wa kudhibiti matatizo ya hali ya anga, wanachuo hawa walipigwa jeki na shirika la Climate-U Network.

Shirika hili kuunganisha vyuo vikuu duniani vinavyosfanya utafiti wa kuangazia mabadiliko ya tabianchi (hali ya hewa).

Daniel anaendelea kuomba serikali za kaunti na ile ya kitaifa kuwasaidia kustawisha ubunifu wao licha ya kujaribu kuwafikia bila mafanikio.