Habari

Wanafunzi kukaa nyumbani kwa siku zingine 30

April 26th, 2020 2 min read

ELIZABETH OJINA na VITALIS KIMUTAI

SERIKALI imeongeza muda wa likizo ya shule za msingi na upili kwa siku 30.

Hatua hii inazidi kuibua maswali kuhusu hatima ya elimu, hasa kwa wanafunzi waliokuwa wanajiandaa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) na ule wa Upili (KCSE).

Ratiba ya awali ilihitaji shule zifunguliwe Mei 4 kwa Muhula wa Pili. Katika Muhula wa Kwanza, shule zilifungwa mapema kabla watoto wafanye mitihani baada ya kisa cha kwanza cha virusi vya corona kutangazwa nchini.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema Jumapili likizo hiyo ya ziada itaanza kuhesabiwa kuanzia Mei 4.

Alisema kufikia sasa, serikali haijaamua kuahirisha KCPE na KCSE.

“Kila mtoto atapewa nafasi kujirudishia nafasi aliyopoteza kabla mitihani ifanywe,” akasema Prof Magoha.

Chama cha Walimu cha KNUT, kilitaka shule zifunguliwe kwa awamu ili kuruhusu watahiniwa kujiandaa kwa ajili ya KCPE na KCSE.

Kwa upande mwingine, chama cha KUPPET kinapinga pendekezo hilo kikisema hatua hiyo itaweka maisha ya walimu na wanafunzi katika hatari.

Chama cha Knut pia kinataka Wizara ya Elimu kutenga fedha zitakazotumiwa kuwalipia karo wanafunzi kutoka familia zisijojiweza shule zitakapofunguliwa baada ya janga la corona.

“Serikali ianze kwa kufungua shule kwa ajili ya watahiniwa wa KCPE na KCSE, kisha wanafunzi wengine watafuatia baada ya janga la corona,” akasema Katibu Mkuu wa Knut, Bw Wilson Sossion.

“Serikali ihakikishe kuwa watahiniwa wanaorejea shuleni wanazingatia masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kama vile wanafunzi kutokaribiana, kunawa na kuvaa maski. Shughuli kama vile michezo, ziara, mikutano ya kwaya na mikusanyiko mingineyo ipigwe marufuku,” akasema Bw Sossion.

Alisema viongozi wa Knut na wakuu wa shule za msingi na sekondari wanafaa kujumuishwa katika kutengeneza mwongozo utakaotumiwa na watahiniwa watakaporejea shuleni.

Alisisitiza kuwa mpango wa elimu kupitia intaneti, redio na televisheni uliozinduliwa na Wizara ya Elimu umekosa kuzaa matunda.

Bw Sossion alisema kuwa wanafunzi kutoka vijijini na familia maskini hawajawa wakinufaika na masomo yanayofundishwa kupitia intaneti na runinga.

Alitaka shule zinyunyuziwe dawa ya kuua viini kabla ya wanafunzi kuruhusiwa kurejea.

Pia alipendekeza kuwa madawati yasiwekwe karibu ili kuzuia uwezekano wa wanafunzi kuambukizwa virusi vya corona.

“Wanafunzi wanaopatwa na dalili zinazofanana na zile za corona watibiwe katika hospitali tofauti na watu wazima. Kadhalika, watu kutoka nje wapigwe marufuku kwenda shuleni,” akasema.

Kwa upande mwingine, Katibu wa Kuppet tawi la Kisumu, Bw Zablon Awange, alisema kuwa chama hicho hakiungi mkono pendekezo la kuwataka watahiniwa wa KCPE na KCSE kurejea shuleni kujiandaa kwa ajili ya mitihani ya kitaifa.

“Hatuna hakika kwamba virusi vya corona havitasambaa shuleni? Hatufai kuhatarisha maisha ya walimu na wanafunzi kwa sababu tunahitaji kukamilisha silabasi,” akasema Bw Awange.

Wiki iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali inafanya mipango ya kuhakikisha watahiniwa wanajiandaa kikamilifu.