Habari

Wanafunzi kutoka Kenya walio China wasema serikali imewatelekeza

February 7th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

CHAMA cha wanafunzi wa Kenya walio China (KENSWA) kimelaumu serikali kwa kuwatenga na kuwatelekeza watu katika nchi hiyo kukiwa na hatari kubwa wao kuambukizwa virusi vya Corona.

Chama hicho kimeiomba serikali kuwaondoa wanafunzi wote walio katika mji wa Wuhan ambayo imeathirika zaidi na virusi vya Corona.

Wanafunzi hawa walilaumu ubalozi wa Kenya huko China kwa kukosa kujibu barua waliotuma mnamo Januari 31 wakielezea changamoto zao.

Katika barua ya pili walioielekeza kwa Waziri wa Mambo ya Nje Bw Macharia Kamau mnamo Februari 5, 2020, viongozi wa wanafunzi hao walirejelea kuwa hali imezidi kuwa mbaya na wana wasiwasi mwingi na pia wazazi wao nyumbani wamejawa na hofu sana.

Pia walisema wana njaa kwa kuwa kupata mahitaji ya kila siku imekuwa changamoto.

Wanafunzi hawa walisema wako tayari kupimwa na hata kutengwa kwa siku 14 baada ya kuwasili nchini.

Homa hiyo ya China inayosababisha na virusi vya Corona ilizuka mnamo Desemba 2019 na kufikia Februari 7, 2020, watu 636 wamepoteza maisha na 31,000 wameambukizwa. Hii ni kulingana na takwimu za Tume ya Afya ya China.

Mnamo Januari 31, 2020, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitangaza virusi vya Corona kuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu na ambalo dunia nzima ilifaa kuchukua hatua za dharura kukabili.