Wanafunzi mtaa wa mabanda wakiuka hali ngumu na kufanya vyema

Wanafunzi mtaa wa mabanda wakiuka hali ngumu na kufanya vyema

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

WANAFUNZI watano katika mitaa ya mabanda ya Mukuru walikiuka hali ngumu ya mazingira waliyosomea na kuzoa alama zaidi ya 400 kwenye mtihani wa KCPE 2021.

Akiwapongeza na kutoa ushauri nasaha jana, mkurungenzi mkuu wa Mukuru Promotion Centre (MPC), Mtawa Mary Killeen aliambia Taifa leo watoto hao waliathirika wakati wa mikasa ya moto mtaani. Isitoshe, Mtawa Killeen aliongeza kwamba mafuriko mwaka jana, janga la Corona, ubomozi wa nyumba kupisha ujenzi wa barabara sawia na ukosefu wa stima hazikuwazuia kujibidiisha masomoni na kufanya vyema katika mtihani wa KCPE mwaka jana.

Watoto hao walikuwa ni Fidel Okatch aliyezoa alama 400, Brian Musyoki aliyepata alama 401 na Samuel Isavwa aliyeibuka na alama 409. Wengine ni Gregory Ouma aliyepata alama 410 na Sharp Felix aliyezoa alama 417. Watoto hawa watano walisomea katika shule nne za umma zilizo ndani ya mitaa mbalimbali katika maeneo ya Mukuru.

Zaidi ya hayo, shule hizo zinafadhiliwa na MPC chini ya usimamizi wa Sisters of Mercy-Kenya Chapter. Mtawa Killeen alisema Okatch alisomea shuleni ya msingi ya St Catherine, Musyoki akijiunga na shule ya msingi ya St Bakhita huku Sharp akisomea katika shule ya msingi ya St Elizabeth.

Kando na hayo, Isavwa na Ouma walikuwa pamoja katika shule ya msingi ya Mukuru. Kuhusu maskani yao, Okatch alikuwa akitoka kila asubuhi saa kumi na moja asubuhi kutembea kutoka mtaa wa Muthurwa hadi St Bakhita South ‘’B’’ iliyo umbali wa kilomita tano.

Musyoki ni mkazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kamongo kwenye wodi ya Landi Mawe ilhali Felix ni mkazi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Lunga Lunga kwenye wodi ya Viwandani, eneo bunge la Makadara.

Vilevile, Ouma na Isavwa ni wakazi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba ulioko katika kaunti ndogo ya Starehe. Masuala mengine kuhusu watoto hawa ni kwamba waliokuwa mabingwa kutoka idadi ya watahiniwa 792 kutoka kwa shule nne za msingi zinazothaminiwa na MPC.

Babake Gregory, Bw John Odhiambo, 58 aliye kadhalika baba wa watoto 10, aliambia Taifa Leo kwamba Gregory alikuwa mtoto mwerefu tangu akiwa chekechea. “Ni mvulana mtulivu, aliye na nidhamu nzuri na anafuata nyayo za kakaye mkubwa aliye chuoni kikuu cha Kenyatta. Hakuwa na baadhi ya vitabu huku tukiishi gizani baada ya kukosa umeme mtaani japo alifanya vizuri katika mtihani wake,” Bw Odhiambo akasema.

Kadhalika, Bw Jim Sharp, 42 ambaye ni babake Felix Sharp alisema mwanawe ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita. “Mwanangu alisomea katika mtaa ulio na makelele, ukosefu wa stima na changamoto za mafuriko. Hata hivyo, alitegemea usaidizi wa vitabu alivyoomba kutoka kwa marafiki tofauti,” Bw Sharp akasema.

Changamoto ya Bw Sharp ni kwamba anafanya vibarua vya Jua Kali na anatarajia kupata changamoto ya ukosefu wa karo. Kwa jumla yatafuatayo ni azimio ya wanaunzi wote watano na uraibu wao mtawalia. Okatch angependa kusomea uhandisi wa stima na ni mchoraji shupavu.

Musyoki angependa kuwa mhandisi wa ujenzi au kuwa rubani bali na kupenda kupaka rangi. Isavwa huhusudu kuongelea na anatarajia kuwa mhandisi katika siku za usoni. Ouma hupenda kambumbu huku Sharp akipendelea kusoma vitabu vya riwaya kando na kuwa mhandisi wa elektroniki na msomi wa nyota na masuala ya angani.

You can share this post!

Bunge lajadili kwa uzito changamoto ya uhaba wa mafuta

Liverpool guu moja ndani ya 4-bora UEFA baada ya kutandika...

T L