Kimataifa

Wanafunzi nchini Zimbabwe waweka rekodi mpya ya Guinness

May 29th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUNDI la wanagenzi nchini Zimbabwe sasa limeweka historia kwa kuhakikisha limeingia katika orodha ya Rekodi za Dunia za Guinness.

Kulingana na ripoti, wanafunzi 222 walivunja rekodi wakati wa hafla ya ZiMarimba iliyoandaliwa Mei 25 katika shule ya Prince Edward, jijini Harare.

Wanafunzi hao walicheza pamoja ngoma katika kundi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani, na kuvunja rekodi iliyowekwa na wanafunzi 108 kutoka jimbo la Oaxley, Brisbane, Australia mwaka 2016.

“Washindani 222 hao walicheza pamoja wimbo maarufu ya marimba, Manhanga Kutapira, kwenye ala za marimba kwa dakika tano, na kuipa Zimbabwe nafasi kwenye rekodi za dunia,” ikaripoti¬† face2face Africa.

Akihutubia wanahabari baadaye, kiongozi wa masogora hao Mpiwa Gwindi alisema kuwa “ilikuwa inaongoa, sitawahadaa. Ilinifurahisha sana kusikia sauti hiyo.”

“Rekodi imevunjwa na sasa na nina bashasha tele,” akasema mmoja wa wanachuo walioshiriki kwa densi hiyo.

Taifa hilo pia limeweka rekodi ya Guinness kwa mradi mkubwa zaidi wa kufuga ndovu, ambapo ndovu 500 walisafirishwa kilomita 250 Agosti 1993.