Habari Mseto

Wanafunzi vyuoni kutumia kadi za kidijitali kupokea mikopo ya HELB

August 15th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Jumla ya wanafunzi 69, 151 ambao watajiunga na vyuo vikuu kuanzia Septemba mwaka huu watapokea pesa za mkopo wa HELB kwa kutumia kadi za kidijitali, Waziri wa Elimu Bi Amina Mohamed ametangaza.

Bi Mohamed Jumatano alisema hatua hiyo ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa utumiaji wa kadi hizo unapokelewa na vyuo vyote vya elimu nchini.

Aidha, waziri huyo aliamrisha vyuo vya masomo ya kiufundi (TVET) kuanzisha mfumo huo kufikia Disemba 31.

“Kadi hizo zitahakikisha utumiaji wa pesa ambazo zimewekezwa katika sekta ya elimu na serikali ni wa manufaa. Pia ninavikumbusha vyuo vikuu kuwa matumizi ya kadi hizi sharti yaanzishwe Septemba mwaka huu,” akasema Bi Mohamed.

Waziri huyo alisema haya wakati wa kikao na waandishi wa habari katika makao makuu ya bodi ya HELB jijini Nairobi.