Habari Mseto

Wanafunzi wa Kenya waliokwama Sudan kurudishwa nyumbani

June 16th, 2020 1 min read

WACHIRA MWANGI

Angalau wanafunzi 120 wa Kenya waliokwama Sudan kutokana na makataa ya kutoingia humu nchini kutokana na janga la corona wamepata matumaini ya kurudi nyumbani hivi karibuni baada ya mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na wahisani kusikia kilio chao wakiomba kurudishwa nyumbani.

Wanafunzi hao ambao wanasema kwamba fedha zimewaishia huku wengine wakipatwa na masaibu, waliomba usaidizi wakutanishwe na familia zao.

Wanafunzi wengi ni wa kufadhiliwa hivyo hawana uwezo wa kujilipia tiketi inayongarimu kati ya Sh 56,000 na Sh58,000.

Huku akihutubia wazazi na jamaa za wanafunzi hao waliokwama Sudan Bw Nassir alisema kwamba mipango ipo ya kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wamerudi nchini.

Bw Nassir alisema wanafunzi hao lazima wapimwe virusi vya corona ndipo waweze kuruhusiwa kuingia humu nchini na kuepuka karantini ya lazima ya siku 14.

Aliongeza kwamba pamoja na mafariki wake wametoa Sh1 milioni ili kuwatoa wanafunzi hao Sudan.