Habari Mseto

Wanafunzi wa MKU wafadhiliwa kujiendeleza katika ubunifu

May 7th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) waliojiunga na vikundi mbalimbali vya masomo wamefadhiliwa kifedha ili kujiendeleza katika ubunifu.

Vikundi sita viliteuliwa na kamati ya bodi ya chuo hicho na kufadhiliwa kwa takribani Sh3 milioni huku kila kimoja kikipewa Sh200,000.

Mwenyekiti wa bodi ya MKU Prof Simon Gicharu alisema vikundi hivyo vilionekana kuwa na ubunifu wa kujiendeleza kimasomo na ndiyo maana wametambulika na chuo hicho kama wenye maono.

Mwenyekiti wa bodi ya MKU Profesa Simon Gicharu (katikati amevalia shati jeupe) akiwa na wanafunzi waliofadhiliwa kwa kupewa fedha za kujiendeleza katika ubunifu wao wa kimasomo. Pamoja naye ni maafisa wengine wa bodi ya chuo hicho. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tunao wanafunzi wengi wabunifu katika masomo yao na vikundi hivyo ni mifano bora kabisa. Kuna matumaini ya kwamba watajizatiti na kujiendeleza zaidi kwa kutumia fedha hizo vizuri,” alisema Prof Gicharu.

Vikundi hivyo viliteuliwa na kamati ya bodi ya chuo hicho iliyoongozwa na Evans Mwiti na Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Stanely Waudo.

Ushindani mkali

Prof Waudo alitoa changamoto kwa walionufaika kwa kuwahimiza wawe wabunifu katika masomo yao ili kujiweka imara katika ushindani mkali wa masomo ulimwenguni.

“Ninawahimiza muwe na maono katika jambo lolote mnalotenda. Ni muhimu liwe limefanyiwa utafiti wa kutosha ili kuthibitisha uhalali wake,” alisema Prof Waudo.

Prof Gicharu ambaye ndiye mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho aliwahimiza walionufaika kuwa watu wenye kuzalisha ujuzi wa hali ya juu pamoja na kuwa wabunifu ili mambo yote ya kielimu wanayoangazia yawe ya kuaminika na wote.

“Ninaelewa mtihani ulio mbele yenu ni mzito lakini mkishirikiana vyema kwa kujiamini, bila shaka kila kitu kitafanikiwa,” alisema Prof Gicharu.

Baadhi ya makundi ya wanafunzi waliotambuliwa ni Catholic Association, ambapo ubunifu wao ulihusu mambo mengi kuanzia uchumi hadi lugha.

Akiwapongeza wanafunzi hao Prof Gicharu alisema ufadhili uwe na mwongozo wa kuwapa mwelekeo wa kujiendeleza kimasomo.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa mpango kama huo kufanyika katika nchi nzima na aliendelea kusema kuwa chuo hicho kitaendelea kuwapiga jeki wanafunzi wenye maono na ubunifu.