Habari Mseto

Wanafunzi wa TUM kufanya uchaguzi mtandaoni

November 22nd, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

KWA mara ya kwanza, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM) watafanya uchaguzi wa viongozi wao wa mwaka wa 2020 hadi 2021 mtandaoni.

Akithibitisha hilo alipokuwa akizungumza na Taifa Jumapili, Naibu Chansela wa taasisi hiyo, Prof Laila Abubakar alisema kuwa watatumia mfumo huo wa uchaguzi kwa kuwa janga la corona limesababisha wanafunzi wengi kusomea mtandaoni.

Alisema kuwa wanafunzi hao hawajaruhusiwa kufika chuoni hadi pale Wizara ya Elimu itatoa amri hiyo.

“Janga la corona limesababisha mambo mengi kufanyiwa mtandaoni; nasi tumeamua kufanya uchaguzi huo kwa njia hiyo pia,” akasema Prof Abubakar.

Alisema kuwa watafuata mtindo maarufu unaotumiwa na Taasisi ya Mahasibu Nchini Kenya (ICPAK) katika uchaguzi wao.

“Mtindo huo umekuwepo muda mrefu na natumai utatusaidia kufanikisha uchaguzi huo ikizingatiwa kuwa unafanywa mtandaoni kwa mara ya kwanza,” alisema Prof Abubakar huku akiongeza kuwa kamati husika itakutana na kuchagua siku rasmi ya uchaguzi huo kufanyika.

Mgombeaji mmoja, Harun Kipkemoi anayegombea kiti cha Katibu Mkuu alisema kuwa wanaendesha kampeni zao mtandaoni pia.

“Wanafunzi wengine hawaji chuoni, lakini wako makwao wakisomea mtandaoni na pia watahitajika kupiga kura. Tumelazimika kufanya kampeni zetu katika mitandao tofauti za kijamii kama vile Facebook na WhatsApp,” alisema Kipkemoi huku akiongeza kuwa wanasubiri tu siku ya uchaguzi ufanyike.

Mgombea huyo alisema kuwa japokuwa wamelazimika kufanya kampeni mtandaoni ili kuepuka mikutano ya wanafunzi, changamoto ambazo wamepitia ni chache mno, kinyume na matarajio yao.

“Hatukufikiri kuwa tungefanikisha kampeni zetu mtandaoni, lakini mambo yanaendelea vizuri,” akasema.

Uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi katika vyuo vikuu ni kati ya shughuli muhimu ambazo hufanyika katika vyuo vingi humu nchini kila mwaka.